Wajukuu wamshtumu hakimu kuchochea mgogoro wa mirathi

MVUTANO wa kusimamia mirathi ya Zena Shemshadini umechukua sura mpya baada ya wajukuu kumshtumu hakimu mmoja katika Mahakama ya Mwanzo Nzega anachochea mgogoro huo uendelee.
Familia hiyo wameanza kutilia shaka shauri lao wakidai hakimu aliyewahi kuwa katika shauri hilo, Hilda Kibona anashawishi mgogoro.
Hayo yamebainika leo baada ya shauri hilo linaloendelea katika Mahakama ya Mwanzo Nzega mbele ya Hakimu Mfawidhi Abunas Sonyo kuahirishwa hadi kesho.
Marehemu Zena hakuacha watoto,mume, wazazi wala wajukuu, Mahakama iliamuru wahusika waingie kwenye Usuluhishi kwa sababu ni ndugu
Hakimu Sonyo amesema shauri limeahirishwa hadi kesho kwa sababu muhusika mmoja hakuwepo hivyo wanatarajia kufanya Usuluhishi kesho na anaamini wataelewana.
Akijibu tuhuma dhidi ya Hakimu Hilda, Hakimu Sonyo amesema huenda wanao ushahidi lakini anachofahamu hakimu Hilda aliwahi kuwa naye katika shauri hilo na alipenda suala hilo liishe kifamilia.
“Sidhani, hizo labda ni hisia, Hakimu Hilda alikuwa na dhamira waelewane ili jambo liishe kifamilia, kama kuna madai hayo nitafuatili,”amesema Hakimu Sonyo.
Alisema Ijumaa wanatarajia kukutana kwa usuluhishi wakishindwana utaratibu wa kisheria utafuata lakini wanaoendelea mashauri ya mirathi yamalizike kwa njia ya Usuluhishi.
Awali Mahakama hiyo ilitoa uamuzi wa kumteua msimamizi wa mirathi Karim Samji na hakukuwa na pingamizi kutoka kwa wanafamilia lakini baada ya uteuzi aliibuka Salma Mohammed ambaye ni mtoto wa mdogo wa marehemu akafungua shauri akiomba kuteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi hiyo, mvutano ulianzia hapo wakapelekwa kwenye Usuluhishi.
Written by Janeth Jovin