Habari

Wakili Jebra: Uhuru wa Wananchi kujieleza pamoja na kupewa taarifa ni masuala muhimu kwa taifa lolote

Uhuru wa Wananchi kujieleza katika masuala mbalimbali sambamba na kupewa taarifa juu ya masuala muhimu yanayolihusu Taifa, yanatajwa kuwa miongoni mwa masuala muhimu kutekelezwa ndani ya Taifa lolote linaloheshimu na kulinda misingi ya haki za Binadamu.

Hayo yamebainishwa na Wakili Jebra Kambole Septemba 24,2022 wakati wa Mdahalo ulioandaliwa na Jukwa la vijana la ‘Reach Out Tanzania’ uliofanyika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na kuwashirikisha vijana kutoka makundi mbalimbali wakiwemo wanasiasa pamoja na waandishi wa Habari wenye lengo la kujengeana uelewa juu ya masuala yahusuyo Demokrasia.

 

Akizungumza katika mdahalo huo, Jebra alisema Taifa lolote linaloheshimu na kusimamia misingi ya sheria ni lazima lijenge misingi ya wananchi wake kujieleza lakini pia kupewa taarifa za kitaifa zinazowahusu zikiwemo kuhusu njaa, magonjwa na zinginezo kwa kuwa ni haki yao kwa mujibu wa katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa haki kila mwanachi .

““Uhuru wa kijieleza na watu kupata taarifa ni suala muhimu katika Tailfa lolote lile lenye uhuru wa kidemokrasia, ni kawaida sana kuambiwa kuwa hakuna uhuru usio na mipaka, lakini huo mpaka lazima uwe na sheria na siyo tamko la mtu” alisema Jebra

Alisema sheria nyingi ambazo zimewekwa nchini hazipambanui moja kwa moja ni makosa yapi yapo ndani ya vifungu hivyo ili kumfanya yule anayedaiwa kuivunja atambue kosa lake moja kwa moja lakini pia sheria hizo zinapaswa kuwa na adhabu zake zinazoendana na kosa husika.

Alitolea mfano sheria katika vyombo za habari nchini ambapo amesema nyingi zina mapungufu na kusababaisha matokeo yake waandishi na vyombo vya habari kujikuta wakiangukia katika adhabu ambazo msingi wake umetokana na mapungufu yaliyopo ndani ya sheria hizo.

Alisema ni vyema Serikali na Bunge likaona umuhimu wa kuzifanyia marekebisho sheri zote zinazoonyesha kuwa na ‘ukakasi’ wa kutotafsiri vyema kilichozungumzwa ndani yake kwa ajili ya manufaa ya kila mwananchi na hata kizazi kijacho.

Aidha alisema wanasiasa ni miongoni mwa watu wenye nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko nchini kwa Taifa lolote ikiwemo Tanzania kutokana nguvu pamoja na ushawishi walionao katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kijamii, kiuchumi kwani wao ndiyo chachu katika maendeleo ya mataifa hayo.

Katika mdahalo huo ulioongozwa na ‘mada inayosema ‘Wajibu wa Raia kupata haki yake Kidemokrasia’ Jebra alisema hata sera pamoja na sheria mbalimbali zinazoanzishwa na kutumika nchini baadhi zimetungwa na wanasiasa hao kisha kupitishwa na Bunge hatua inayoonyesha wazi nguvu ya kundi hilo katika masuala mengi yanayohusu nchi.

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Ngome ya vijana wa chama cha ACT- Wazalendo Abdul Nondo amesema viongozi wanapochaguliwa wana wajibu wa kutekeleza Sera na sheria ambazo zitakuwa na manufaa kwa wananchi na nchi kwa ujumla.

“Umechaguliwa kuwa Mbunge, kuwa Diwani wajibu wako ni kwenda bungeni, kwenda halmashauri kuhakikisha kwamba unasimama kikamilifu kuwakilisha waliokutuma ili kuhakikisha sheria na Sera mbalimbali zinapitishwa kuwa na manufaa ya wananchi”

 

Aidha Nondo ameongeza kuwa vyama vya siasa nchini vina wajibu wa kuimairisha demokrasia ili hata vinapokuja kushika madaraka iwe ni sababu kuendelea kuimarika kwa demokrasia nchini.

 

“Kwahiyo vyama vya siasa ili kuweza kutengeneza utamaduni wa kuheshimu misingi ya kidemokrasia na Uhuru wa watu kutoa maoni ni lazima vyama vyenyewe vijiimairishe kuwa na demokrasia imara” Ameongeza Nondo

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kanda ya Kati Chadema Aisha Luja alisema katiba mpya ndiyo mwarobaini pekee wa changamoto zinazojitokeza nchini hivyo kuna haja ya kuhakikisha inapatiakana mapema iwezekanavyo kuleta ufumbuzi.

Alisema mapungufu yaliyopo ndani ya katiba hiyo ya Mwaka 1977, ndiyo hasa inayopelekea hadi leo watu wanalaumu na kulalamika kila wakati huku jukumu la kudai katiba hiyo wakiliacha mikononi kwa wanasiasa pekee.

“Kama katiba inayodaiwa hapa ni ya watanzania, kila mtanzania ana wajibu wa kuhakikisha anasimama na kuidai, lakini vyama vya siasa sote bila kujali ukubwa au udogo wetu tunapaswa kudai katiba hiyo kwa sababu sote tunawawakilisha wananchi

 

Naye Mkurugenzi wa Jukwaa la Reach Out Tanzania Kumbusho Dawson amewashukuru wadau waliojitokeza katika mdahalo huo wa Siku mbili huku akiongeza kuwa mapendekezo yaliyotolewa na wadau katika mdahalo huo watahakikisha wanayafanyia kazi pasi na kukiuka misingi ya katiba ya nchi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents