Habari

Wakutana kujadili uundaji wa sera rafiki, kanuni kusaidia kuimarisha biashara ya uzalishaji viwandani

WADAU mbalimbali katika sekta ya viwanda nchini wamekutana ili kujadili juu ya uundaji wa sera rafiki na kanuni zitakazosaidia kuimarisha biashara ya uzalishaji viwandani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika mkutano wa wadau hao ulioandaliwa na Taasisi ya Liberty Sparks, Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa taasisi hiyo, Evans Exaud amesema lengo lao ni kuwezesha uagizaji na usafirishaji wa bidhaa za viwandani bila matatizo, hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi wa Tanzania na ushindani wake katika soko la dunia.

Amesema mkutano huo ni sehemu muhimu ya mradi wa Ujirani Mwema, ambao sasa upo katika awamu yake ya pili na kwamba katika awamu hiyo wanalenga kupitia na kutoa mapendekezo ya kuboresha biashara ya kilimo, biashara ya uzalishaji viwandani, na sekta ya madini katika nchi ya Tanzania.

“Safari yetu ilianza na awamu ya kwanza ya mradi huu, ambapo tuliwashirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo mashirika ya serikali na wizara kama vile Wabunge, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uchukuzi na kikundi kazi. Mashauriano haya ya awali yalikuwa muhimu katika kuweka msingi wa kazi tunayoendelea nayo leo.

“Tunapoingia katika awamu ya pili, wigo wa ushirikiano wetu unapanuka zaidi. Sasa tutashirikisha wizara za ziada, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Nishati na Madini Pamoja na ofisi ya Waziri Mkuu, kuhakikisha kuwa mapendekezo yetu yanakuwa ya kina na yatakayosaidia kushughulikia changamoto na fursa mbalimbali ndani ya biashara ya uzalishaji viwandani na zaidi,” amesema Exaud

Profesa Samwel Wangwe

Aidha amesisitiza kuwa nguvu ya taifa hili ipo katika uwezo wa watu kufanya kazi kwa pamoja katika sekta mbalimbali, viwanda na mipakani hivyo ni muhimu wadau hao kukutana na kujadiliana changamoto zinazowakabili ili ziweze kufanyiwa kazi na wahusika.

Hata hivyo amesema taasisi yao itaendelea kujikita katika kukuza uwezeshaji wa kiuchumi kupitia biashara huru na kubadilishana maarifa, lengo kuu likiwa ni kuchochea ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini nchini Tanzania.

Amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017, wamekuwa wakiamini katika nguvu ya elimu na utafiti katika kuleta mabadiliko chanya kwa jamii, ndiyo maana wamejizatiti katika kutoa suluhisho za kisera ambazo zinachangia katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Naye Profesa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kitengo cha biashara, Samwel Wangwe amesema kuwa miongoni mwa changamoto zinazokabili sekta hiyo ya biashara viwandani ni pamoja na ubovu wa miundombinu, vifungashio hafifu, bidhaa kutokuwa na ubora, upatikanaji wa fedha na masoko kwa ajili ya kuuzia bidhaa.

Amesema ni muhimu kwa wadau hao kukutana mra kwa mara ili kuweza kujadili changamoto hizo na namna zinavyoweza kufanyiwa kazi ili kuweza kuhakikisha sekta hiyo inapiga hatua.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents