Walimu watoro chanzo ufaulu hafifu Songea
![](https://bongo5.com/wp-content/uploads/2024/12/WhatsApp-Image-2024-12-06-at-15.30.01_7b8fb1cb.jpg)
Imebainika kuwa utoro wa walimu ni moja ya vyanzo vinavyochangia ufaulu hafifu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa ya kuhitimu shule ya msingi katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Wilman Kapenjama Ndile katika kikao cha tathmini ya elimu kilichofanyika Desemba 5, 2024 kikihusisha maafisa elimu, waratibu wa elimu kata na vingozi waandamizi wa wilaya hiyo.
Akifafanua maana ya utoro kwa walimu, mkuu wa wilaya alisema kuwa haimaanishi kutokuwepo mazingira ya shule bali kutofundisha vipindi vyote, kama ambavyo inatakiwa.
“Na utoro ni, sio kutokuweo siku nzima. Unaweza kuwepo siku nzima lakini hujafundisha vipindi vyote unavyopaswa kufundisha. Hili ni tatizo kubwa,” alisema Ndile
Aidha alifafanua kuwa, walimu badala ya kufundisha wamekuwa wakitumia muda wa kazi kufanya mambo yao binafsi ikiwemo kilimo na uvuvi, huku baadhi wakichukua watoto kwenda kuwasaidia.
Akielezea athari ya hatari ya utoro wa walimu, Ndile alisema kwanza mwalimu mtoro hawezi kudhibiti watoto watoro, pili, walimu wa aina hiyo wanaiibia serikali kwa kutofanya kazi kwa muda unatakiwa.
Ndile alisema: “Kazi lazima ufanye masaa nane. Leo asubuhi nilikuwa naongea na Mwenyekiti, ananambia anaye mwalimu mmoja mmoja pale kijijini kwake masaa mengi anatumia shambani kwake, mbaya zaidi na tena mbaya zaidi anaenda mpaka na watoto.”
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Vijijini, Elizabeth Magingo alikemea tabia ya baadhi ya maafisa wa elimu wa kata ambao wamegeuza pikipiki walizopewa kuwawepesishia kazi na kuzifanya bodaboda.
“Nina taarifa kutoka kwa raia wema kwamba kuna baadhi ya pikipiki ambazo zimetolewa na serikali zinaonekana zikifanya kazi ya bodaboda. Sasa wewe mratibu kata unazungukaje?” alihoji na kuonya kuwa akikamata pikipiki inayotumika isivyo hatamrejeshea muhusika,”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea Vijijini, Mennas Komba alimtaka Afisa elimu kama ameshindwa kuwadhibiti baadhi ya walimu wakorofi alikabidhi baraza la madiwani liwashughulikie.
Written by Angel Kayombo, Ruvuma