‘Waliwaua vijana wote’ – yanachunguzwa madai ya mauaji katika mji unaoshikiliwa na waasi

‘Waliwaua vijana wote’ – BBC inachunguza madai ya mauaji katika mji unaoshikiliwa na waasi

Dakika za mwisho za Freddy Mukuza zilishuhudiwa na rafiki yake, ambaye alikuwa amesimama bila uwezo wa kumsaidia, umbali wa mita 50 (futi 160).
Aliposikia kwamba Freddy amepigwa risasi – na waasi wa M23 – yeye na wengine walikimbilia eneo la Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
“Tulipofika tulimkuta Freddy bado anapumua, tukataka kumchukua, lakini M23 hawakuturuhusu,” anasema rafiki huyo tunayemuita Justin.
“Tuliposisitiza, walifyatua risasi ardhini kana kwamba wanasema: ‘Ukithubutu kuvuka eneo hili, tutakuua pia wewe.”
Kwa hivyo walilazimika kukaa mbali, kwani Freddy, 31, alivuta pumzi yake ya mwisho. Hapo ndipo M23 walipowaruhusu kumsogelea na kuuchukua mwili wake.
Muda mfupi kabla ya mauaji hayo, malori matatu yaliyojaa wapiganaji wa waasi yalikuwa yamefika katika mtaa wa karibu na Freddy – Kasika.
Ilikuwa takriban saa 15:00 siku ya Jumamosi tarehe 22 Februari – karibu mwezi mmoja baada ya kundi la waasi kuteka mji wa Goma kwa kasi ya ajabu mashariki mwa nchi.
Ndani ya saa moja hivi, kati ya watu 17 na 22 walikuwa wameuawa, wengi wao wakiwa vijana, kulingana na vyanzo vyetu.
Tumekusanya maelezo ya kina kutoka kwa wakazi, ambao hawawezi kutambuliwa, kwa sababu ya ulinzi wao wenyewe.
Tuliwaandikia M23 ili kupata maoni yao juu ya madai kuwa walifanya mauaji makubwa katika kitongoji hicho. Lakini hawakujibu.
Maafisa huko Kasika hawajatoa idadi ya waliouawa, na kuna matarajio machache au hata hakuna kabisa ya uchunguzi huru wa uhalifu kuhusu kile wakazi wanakiita mauaji.
Lakini wenyeji wanasisitiza kuwa M23 ndilo kundi pekee lenye silaha ambalo linaweza kufanya kazi humo kwa uhuru, na kuua watu kwa kuwapiga risasi mchana kweupe huko Goma.
Tangu kuchukua mji huo mwishoni mwa Januari, waasi wamekuwa wakiudhiti. Katika siku 18 tulizokaa hapo, mamlaka yao ndio ilikuwa na nguvu yote.
Wameshutumiwa siku za nyuma kwa kutekeleza ukatili katika maeneo mengine.
Waasi waliojihami kwa silaha nzito hawachukui hatua peke yao.
Wanaungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, kulingana na Umoja wa Mataifa na Marekani. Hata hivyo, Rwanda inakanusha madai haya ingawa haikanushi tena kuwa na wanajeshi wake nchini DR Congo, ikisema wako huko kujilinda.
Inaaminika M23 walimlenga Kasika kwa sababu ya kambi ya zamani ya jeshi la Congo katika eneo hilo.
Kambi ya Katindo sasa imefungwa lakini baadhi ya wanajeshi na familia zao wamesalia wilayani humo.
“Si wanajeshi wote waliweza kukimbia,” mkazi wa eneo hilo anaelezea. “Baadhi walitupa bunduki zao na kujiunga na wenyeji ambako wanaishi kwa ujirani.”
Lakini Freddy Mukuza alikuwa raia – baba mwenye mke na watoto wawili, akijitahidi kujikimu. Alijitafutia riziki kwa kufanya kazi ya bodaboda.
Pia alikuwa mwanaharakati na mtunzi wa nyimbo za muziki wa kufoka foka kuhusu matatizo mengi katika nchi yake – nchi ambayo ni tajiri kwa madini lakini watu wake ni miongoni mwa maskini zaidi duniani.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inajulikana kama mahali pa rushwa na ukosefu wa utulivu – na wa migogoro, iliyoanzia miaka 30 iliyopita.
Hilo ni ikiwa nchi na mateso yake yatakumbukwa hata japo kidogo tu.
Unyanyasaji wa kijinsia umeenea. Serikali ni dhaifu.
Kulikuwa na mengi kwa muziki wa Freddy.
Moja ya nyimbo zake inaitwa Au Secours (ikimaanisha msaada kwa Kifaransa).
“Nani atakuja kuwasaidia watu hawa? Nani atakuja kuwasaidia wanawake hawa waliobakwa? Nani atakuja kuwasaidia wanaume hawa wasio na ajira?… Watu wako hatarini, hawana chakula cha kutosha. Wao [mamlaka] wananunua magari aina ya jeep.”
Siku ya kifo chake, Freddy alikuwa akihamia nyumba mpya ya kupanga huko Kasika. Shemeji yake alikuwa akimsaidia kuweka turubai juu ya paa.
Mke wa huyo shemeji yake naye alikuwepo akiitayarisha nyumba kwa ajili ya familia ya Freddy. Waliposikia milio ya risasi, walikuwa ndani na kukimbilia kufunga mlango, lakini walionekana na M23.
Waasi hao waliwapiga risasi na kuwaua nao, kwa mujibu wa rafiki yake Justin.
Tangu wakati huo, Justin ametoroka nyumbani akiacha familia yake ikiwa inaishi kwa mboga mboga na matunda tu. Chai sasa ni anasa ambayo hawawezi kumudu.
Amewasimamisha watoto wake kwenda shuleni, kwa kuhofia wanaweza kuchukuliwa kutoka madarasani mwao na M23 na kusajiliwa kwa nguvu kama wapiganaji.
“Tunaamini ni muhimu zaidi kwamba waendelee kuwa hai,” anasema.
Ulimwengu wake umekuwa mdogo sana. Kuna hofu kila wakati kwamba waasi wanaweza kurudi kuwawinda vijana.
Kuona tu moja ya lori lao la kubebea mizigo barabarani huwafanya wenyeji kukimbia, anasema.
Siku hizi ni nadra sana kukuta kikundi cha vijana wakizungumza pamoja, anatuambia, na majirani hawashirikishani tena changamoto za mamlaka kama walivyofanya kabla ya waasi kuchukua mamlaka.
“Hapo awali, kulikuwa na utawala mbaya, lakini tulikuwa huru,” anasema. “Kulikuwa na ubadhirifu. Kulikuwa na usimamizi mbaya na tulizungumza kuhusu hilo. Tulipata fursa ya kwenda mahakamani. Leo, kuna utawala mbaya, lakini tunaishi kwa hofu na ukimya.”
Justin anazungumza nasi kwa sababu anataka Freddy Mukuza akumbukwe, na anataka ulimwengu wa nje ujue kuhusu maisha na vifo vinavyotokea chini ya M23.
Chanzo cha picha, AFP
Tangu mauaji hayo, Kasika imegubikwa na hofu. Waandishi wa habari wa eneo hilo hawajaripoti habari hiyo.
Lakini video inayotikisika iliwekwa kwenye mitandao ya kijamii siku iliyofuata, 23 Februari, ambayo inaonekana kuonyesha baadhi ya waathiriwa: miili 10 inaonekana – imetupwa kwenye rundo lililochanganyika, katika jengo ambalo halijakamilika. Haijulikani ikiwa yeyote kati ya waliokufa ni wanajeshi.
Hakuna aliyevaa sare na hakuna dalili ya uwepo wa silaha yeyote.
Kwa nyuma mayowe yanasikika. Mwanamke mmoja anarudia tena na tena: “Idadi yao ni 10,” anapotoka kwa mwili mmoja hadi mwingine.
“Watatumaliza sote,” anasema. “Waliwaua vijana wote hawa, yule sio Junior? Nafkiri ni yeye. Ni mjenzi wa nyumba.”
Bila video hiyo, habari za mauaji hayo huenda zisingeenea zaidi ya kitongoji.
Lakini picha hizo zilikuwa na nguvu ya kushtua, hata kwa viwango vya vurugu zinazoendelea DR Congo.
Vyanzo vyetu vinasema ni kweli. Mmoja alithibitisha kuwa eneo lililoonyeshwa ni Kasika.
Alitembelea sehemu hiyo baada ya miili kuondolewa. Na akamtambua mmoja wa wale walioonekana akilia kwenye video, kutoka jirani na hapo.
Vyanzo vyetu viwili vinasema mdogo zaidi kufariki Kasika alikuwa mvulana mwenye umri wa miaka 13-14. Kijana huyo alikuwa ndani ya nyumba yake mwenyewe, akijificha nyuma ya dada zake.
“M23 wakasema: ‘Ikiwa mvulana huyu hataandamana na sisi, tutawaua ninyi nyote,” mtu mmoja alituambia.
Kisha mvulana huyo akatoka kwenda kufuata kifo chake.
Baada ya wiki kadhaa, ni wachache tu ambao wamethubutu kuzungumza. “Hakuna mtu anataka kuwa atakayefuata kuuawa,” John anasema.
Familia zilizofiwa zimefanya mazishi ya haraka- bila maombolezo ya kawaida nyumbani.
“Waasi hawakutaka mazishi yoyote,” amesema mkazi mmoja, ambaye tunamwita Deborah. “Hawakutaka hata watu kulia, tulidhani wanakuja kuleta amani, badala yake walikuja kutuangamiza. Walichukua kila kitu walichokiona mitaani.”
Wanaume hao walipokuwa wanakusanywa, alijaribu kutoka nje. Waasi waliamuru arudishwe ndani, wakiwa wamemnyooshea bunduki.
Chanzo cha picha, Göktay Koraltan / BBC
Denis Baeni alikuwa akielekea nyumbani wakati waasi hao walipofika Kasika. Aliingia kwenye duka dogo ili kujificha na wengine wachache, vyanzo vyetu vinasema.
Mwalimu wa shule ya msingi alitoa kitambulisho chake mfukoni. Huenda alifikiri hilo lingemuokoa, kwa kuthibitisha kwamba alikuwa raia.
Jirani – anayefahamu kilichotokea kwa sasa tunamwita Rebecca.
“Walisikia sauti kutoka nje ikiuliza: ‘Je, kuna wanajeshi wowote?'” Rebecca anasema. “Walisema hapana lakini M23 waliwatoa nje ya duka.”
Wanaume hao waliambiwa watembee umbali mfupi hadi kwenye nyumba iliyojengwa nusu ambapo “walikuwa wamekusanywa kwa ajili ya kuuawa”.
“Kulikuwa na milio ya risasi,” anasema. “Ilikuwa karibu sana. Kulikuwa na watu 21 waliouawa kwa wakati mmoja kutoka eneo jirani. Wengi walikuwa wakipita tu.”
Rebecca anasisitiza kuwa wote walikuwa raia. “Hakuna hata mmoja aliyekuwa mwanajeshi,” anasema.
Denis ameacha watoto wawili ambao alikuwa akiwalea peke yake.
Kifo sio hatari pekee inayokodolea wenyeji macho, lakini pia wanakabiliwa na hatari ya kusajiliwa kuwa wapiganaji – kwa hiari au vinginevyo.
“Siku hizi wanaume wanapaswa kuwa nyumbani ifikapo saa 17:30,” anasema Rebecca. “Kufikia 18:00 ni giza, na wanaweza kukuchukua kwa urahisi sana.”
Chanzo cha picha, AFP
Huku familia za Kasika zikilazimika kutozungumzia huzuni yao, M23 wanaendelea na msako wao mashariki mwa DR Congo.
Baada ya Goma, walidhibiti jiji la Bukavu katikati ya Februari. Wametishia kwenda hadi mji mkuu, Kinshasa, umbali wa kilomita 1,600 (karibu maili 1,000).
Wanadai wao ni wanamapinduzi wanaopambana na taifa lililoshindwa, na kutetea haki za Watutsi walio wachache.
Hata hivyo, makundi ya haki za binadamu yanatoa taswira tofauti kabisa.
Wamelishutumu kundi hilo lenye silaha kwaunyanyasaji tangu kuanzishwa kwake mwaka 2012 – ikiwa ni pamoja na mashambulizi yaliyopangwa katika maeneo ya raia, ubakaji na “mauaji”. Madai hayo yameandikwa katika ripoti kadhaa.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na BBC, kiongozi wa waasi, Corneille Nangaa, alijibu. Anaongoza muungano wa vyama vya siasa na wanamgambo – unaoitwa Muungano wa Congo River – unaojumuisha M23.
“Sikuona ripoti,” alisema. “Siwezi kujibu ripoti ambayo sikuisoma”. Pia alisema hana wasiwasi na madai hayo.
Alipoulizwa kwa nini hakusoma ripoti hizo, alisema: “Nipe moja, nitaisoma.”
Nangaa, mkuu wa zamani wa tume ya uchaguzi ya DR Congo, anaonyeshwa kama waasi wasio na silaha wala tishio, lakini serikali ya Congo inatoa zawadi ya $5m (£4m) kwa habari zitakazowezesha kukamatwa kwake .
Waasi hawako peke yao katika historia ya ukatili. Hali hiyo hiyo inatumika kwa jeshi la Congo, na kwa vikundi vingine vingi vilivyo na silaha mashariki mwa DR Congo.
Lakini M23 sasa ndio mamlaka pekee katika baadhi ya sehemu za mashariki, na mamilioni ya Wakongo wako chini ya huruma yao.
Tulipokuwa tukizungumza na mkazi mmoja wa Kasika, mkewe alimpigia simu na kumtaka aje haraka kumchukua mtoto wao wa miaka minane shuleni.
Hofu ilikuwa ikitanda kwa sababu ya ripoti kuwa M23 walikuwa wakiwachukua watoto kutoka madarasani mwao.
Alimrudisha mtoto wake nyumbani salama lakini anahofia siku zijazo.
“Sote tumepatwa na kiwewe. Walisema walikuja kutukomboa,” alisema. “Lakini sasa ni kama wanatuchukua mateka.”
cc:BBC SWAHILI