Habari

Wanawake Ruvuma waongoza maambukizi Virusi vya Ukimwi

Wanawake mkoani Ruvuma wanaongoza kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi wakiwa ni 43,278 sawa na asilimia 63 huku wanaume wenye maambukizi hayo wakiwa ni 24,959 sawa na asilimia 37.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yenye kauli mbiu ‘Chagua njia sahihi, tokomeza ukimwi’.

Abbas amesema kuwa kutokana na takwimu hizo anawahimizwa wenye maambukizi kutumia dawa za kufubaza virusi hivyo kwani hiyo ndio njia ya pekee kupambana maradhi hayo.

Amesema katika takwimu za jumla za maambukizi mkoani humo, watu 68,237 sawa na asilimia 4.9 ya wananchi wote wamekutwa na maambukizi.

“Hata hivyo kiwango hichi cha ushamiri wa virusi vya ukimwi kimeshuka ukilinganisha na takwimu za mwaka 2017 ambapo yalikuwa 5.6. Takwimu zaidi zinaonesha kuwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 15 wenye maambukizi ni 2,382 sawa na asilimia 3.5,” amesema

Akizungumza awali mwakilishi wa Wizara ya Afya katika maadhimisho hayo, Catherine Joakim alipongeza uongozi wa mkoa wa Ruvuma na wananchi wake kwa kupiga hatua kubwa katika kushusha ushamiri wa VVU kutoka asilimia 5.6 hadi 4.9.

Amesema mkoa wa Ruvuma unaongoza kwa upimaji wa VVU ambapo asilimia 82 wanatambua hali zao za maambukizi na asilimia 97 ya walioambukizwa wanatumia dawa za kufubaza VVU.

Kilele cha maadhimisho yatafanyika Desemba mosi mkoani Ruvuma chini ya kauli mbiu ‘Chagua njia sahihi, tokomeza ukimwi’ ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais Prof Isidory Mpango.

Written by Angel Kayombo, Ruvuma

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents