Habari

Wanolewa kuhusu namna bora ya upandikizaji mimba

KITUO cha Upandikizaji Mimba cha Kairuki Hospital Green IVF (KHGIVF), kimeendesha mafunzo kwa madaktari wa hospitali mbalimbali kuhusu namna bora ya upandikizaji mimba.

Mafunzo hayo yametolewa leo kwenye kituo hicho, Bunju A Mianzini jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na madaktari zaidi ya 50 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kituo cha KHGIVF ambacho kilizinduliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi hivi karibuni kiko chini ya Mtandao wa Elimu ya Afya Kairuki (KHEN).

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dk. Clementina Kairuki, Bunju A Mianzini, wakati wa mafunzo kwa madaktari mbalimbali kuhusu namna bora ya upandikizaji mimba.

Dk. Clementina amesema wanawake wengi wameshafanyiwa upandikizaji mimba kwenye kituo hicho na kufanikiwa kupata watoto lakini wengi walijifungulia kwenye hospitali mbalimabli na wengine nje ya nchi na wamekuwa wakifuatilia hali zao za afya.

“Tunawafuatilia na wanaendelea vizuri sana watoto na mama zao na watanzania hawana sababu ya kuhangaika kutumia gharama kubwa kwenye mataifa ya Ulaya kwasababu huduma hii sasa inapatikana hapahapa nchini na yenye mafanikio makubwa sana,” amesema

Amesema kituo hicho kimekuwa ikipokea wanawake wengi wengine wakitokea mikoani ambao hufanyiwa huduma hiyo kwa siku moja na kisha kurudi kuendelea na shughuli zao za kawaida kwenye maeneo yao.

Dk. Clementina amesema wakati wa uzinduzi wa kituo hicho hivi karibuni waliahidi kwamba hakitakuwa cha kutoa tiba tu bali kitatumika kutoa mafunzo kuelimisha watanzania na kubadilisha uzoefu na wanataaluma wa tiba kuhusu namna bora ya kupandikiza mimba.

“Tumeanza leo kuwapa mafunzo madaktari wenzetu kutoka hospitali mbalimbali nchi nzima kuhusu upandikizaji mimba ili Tanzania isonge mbele kwenye tiba ya upandikizaji mimba,” amesema na kuongeza

“Tunataka kutoa mwelekeo sahihi kuhusu hii tiba ili kama kuna dhana potofu watu wajue ili tufikie wenzetu walipofikia kwenye tiba hii na tunatarajia angalau tufanye mafunzo kama haya kwa mwaka mara pili,” amesema.

Dk. George Tryphone ambaye ni Meneja wa Mabara ya Upandikizaji Mimba wa (KHGIVF), amesema tangu waanze upandikizaji mimba wamepata mafanikio kwani wanawake wengi wameshapata watoto huku wengine wakiendelea kulea mimba katika hatua mbalimbali.

Amesema kuna baadhi ya wanawake ambao walipandikizwa mimba kwenye kituo hicho na kufanikiwa kujifungua watoto mapacha, watoto watatu kwa mpigo na wengine kujifungua mtoto mmoja mmoja.

Kuhusu mafunzo hayo, Dk. Tryphone amesema jamii bado haijawa na uelewa vizuri kuhusu upandikizaji mimba hivyo wameona ni muhimu kuanza kutoa elimu kwa umma wakiwemo watoa huduma ambao ni madaktari wa hospitali mbalimbali nchini.

“Tumeanza na madaktari tunawapa mafunzo madaktari ili wanaporudi kuwahudumia wanawake wenye changamoto ya kupata ujauzito wawahudumie vizuri katika misingi ile inayohusu msuala ya ugumba ili watatatue changamoto hiyo,” amesema

Amesema suala la kutopata watoto limekua tatizo kubwa nchini kiasi cha watu wengine kulazimika kwenda nchi za nje kupata suluhu ya changamoto hiyo na kulazimika kutumia gharama kubwa na muda mwingi.

Dk. Tryphone amesema kuanzishwa kwa KHGIVF ni ukombozi kwa watanzania wengi ambao walikuwa wakilazimika kusafiri na kutumia gharama kubwa kwani hivi sasa watapata huduma hiyo nchini tena kwa gharama ndogo kulinganisha na nje ya nchi

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents