Habari

Wapigakura wapya Milioni 5.5 kuandikishwa kwenye daftari la kudumu

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imesema kuwa kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, jumla ya wapiga kura wapya Milioni 5.5 wanatarajiwa kuandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.

INEC imesema idadi hiyo ni sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura Milioni 29.7 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/2020.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi INEC Ramadhani Kailima wakati wa mkutano wa tume hiyo na waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Kailima amesema kuwa wapiga kura Milioni 4.3 wanatarajiwa wataboresha taarifa zao na kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari mwaka 2019/20 lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha kuwa wapiga kura.

“ Wapiga kura 594,494 wanatarajiwa kuondolewa kwenye daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye daftari hivyo baada ya uboreshaji inatarajiwa kuwa litakuwa na jumla ya wapiga kura Milioni 34.7,” amesema

Aidha amesema jumla ya vituo 40,126 vya kuandikisha wapiga kura vitatumika katika uboreshaji wa daftari mwaka 2024 ambapo kati ya vituo hivyo 39,709 vipo Tanzania Bara na 417 vikiwa Zanzibar.

“Hili ni ongezeko la vituo 2,312 ikilinganishwa na vituo 37,814 vilivyotumika 2019/2020,” amesema Kailima

Kuhusu uboreshaji wa mifumo ya uandikishaji Kailima amesema mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura umefanyiwa usanifu na kuboreshwa ili kukidhi aina ya BVR Kits za sasa ambazo zinatumia programu endeshi ya androidi.

Amesema hiyo ni tofauti na BVR Kits za awali ambazo zilikuwa zinatumia programu endeshi ya windows.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents