Washauri wanne wa Trump waitwa mbele ya kamati ya bunge Marekani

Kamati ya bunge la Marekani inayochunguza uvamizi wa majengo ya bunge uliotokea Januari 6 mwaka uliopita imetoa hati ya wito wa lazima kwa washauri wanne wa karibu wa rais wa zamani Donald Trump.
Miongoni mwa walioitwa kutoa ushuhuda ni pamoja na mwanasheria wa zamani wa rais Trump. Rudy Giuliani, anayedaiwa kuwa mstari wa mbele kutetea madai ya rais Trump kuwa uchaguzi wa rais wa mwaka 2020 uligubiwa na udanganyifu.
Kamati hiyo ya bunge imesema Giuliani na wenzake watatu wanahusishwa na kushadidida nadharia za wizi wa kura na hata kusaidia juhudi za Trump za kuzuia kuidhinishwa kwa matokeo ya uchaguzi.
Hatua hiyo inaashiria uchunguzi wa kamati ya bunge unatanuka na hata kuwalenga watu wa karibu wa Trump ambaye baadhi ya wanasiasa nchini Marekani wanamtuhumu kuwa alichochea wafuasi wake kuvamia majengo ya bunge mwaka 2021.