Habari

Watanzania Milioni 1.5 wanaishi na virusi vya ukimwi: Utafiti

UTAFITI wa athari za Virusi vya Ukimwi kwa mwaka (Tanzania HIV Impact Survey 2022-2023), umeonesha kuwa watanzania Milioni 1.5 wanaishi na maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.

Utafiti huo wa mwaka 2022-2023 umefanywa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika sekta ya afya.

Akitoa matokeo ya utafiti huo katika mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake (TAMWA) kwa kushirikiana na AVAC, Mchumi Mwandamizi na Kaimu Meneja sehemu ya Mipango na Bajeti TACAIDS, Renatus Mukasa amesema asilimia 80 ya maambukizi ya virusi hivyo ipo kwenye kundi la vijana hususani wenye miaka 15 hadi 24.

Amesema kwa mujibu wa tafiti hizo zimeonesha katika kundi hilo kubwa la vijana la asilimia 80, asilimia 40 ni wasichana balehe na wanawake vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, wanaume vijana, wanawake wanaofanya biashara ya ngono na watumiaji wa dawa za kulevya hasa wale wanaojidunga sindano.

Mkurugenzi Mtendaji Shirika lisilo la Kiserikali la DARE, Dk. Lilian Benjamin

“Kwa mujibu wa takwimu hizi utaona kundi hili la vijana linaathirika zaidi,” amesema Mukasa

Amesema Serikali imeendelea kuhakikisha inaandaa huduma rafiki katika vituo vyote vya kutolea huduma ili kuwahamasisha vijana wengi waweze kupima na kujua afya zao na hali yao ya maambukizi ya virusi hivyo.

“Bila kujua hali ya maambukizi vijana hawa hawataweza kuchua hatua, tunataka wale ambao watapima na kujua afya zao na kama watagundulika kuwa na maambukizi waingie kwenye utaratibu wa tiba na matunzo na wale ambao hawana waweze kuchukua hatua madhubuti za kujizuia na maambukizi,” amesema

Amesema serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuanzisha mijadala na midahalo mbalimbali ya vijana nchi nzima na kila mwaka wanapoadhimisha maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani.

Naye Mkurugenzi Mtendaji Shirika lisilo la Kiserikali la DARE, Dk. Lilian Benjamin anasema asasi za kiraia zimekuwa uti wa mgongo katika mwitikio kwenye jamii mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

“Asasi hizi za kiraia zimekuwa zikifanya kazi kubwa katika jamii kwa kushirikiana na Serikali hasa kuhakikisha jamii zinaweze kupata taarifa sahihi na kuwatengenezea mazingira ambayo watahamasika kupata huduma na kupima VVU,” anasema

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents