Watatu mbaroni kwa kuhujumu miundombinu ya reli ya SGR

WATU watatu wamekamatwa na vipande 396 vya nondo za ukubwa wa milimita 16 zilizokuwa awali zimejengea uzio kuzuia kukatiza wanyama waharibifu akiwemo tembo katika Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Standard Gauge (SGR)
Kamanda wa Kikosi cha Polisi Reli Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Sebastian Mbuta, amesema kuwa kuna uharibifu wa miundombinu ya reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) uliofanywa katika eneo la Ngerengere mkoani Morogoro na Dodoma.
Kamanda amesema kuwa miundombinu hiyo iliyoharibiwa ilikuwa isaidie treni iunganishwe na umeme pindi itakapoanza safari.
“Eneo hilo limenyofolewa na kuacha uwazi mkubwa ambako kumeondolewa vifaa hivyo ikilinganishwa na maeneo mengine yenye nondo ambako kuna mpangilio mzuri,” amesema.
Kamanda amesema kuwa watuhumiwa wametumia maji kuyeyusha ardhi na kuwarahisishia kung’oa nondo na kuacha mashimo.
Kamanda Mbuta, amefika eneo la tukio na kujionea uharibifu huo, sambamba na kufika kituo cha Polisi NgereBashungwangere kushuhudia nondo zilizokamatwa.
ACP Mbuta amesema katika eneo la Ngerengere, tayari wamewatia mbaroni Florah Mbago (39), mkazi wa Kiburumo Ngerengere na Juma Kijiti KItu (66), mkazi wa Mgudeni Ngerengereaa waliokutwa na vipande 17 vya nondo za ukubwa wa milimita 16, mali ya kampuni ya nchini Afrika Kusini ya Rubis, waliopewa kandarasi ya kujenga kilometa 16 za uzio huo wa kuzuia wanyamapori kuvuka upande mmoja kwenda mwingine na kuharibu reli.
Akabainisha mtuhumiwa mwingine Living Emmanuel, (20) ambaye ni fundi wa kujenga uzio na mkazi wa Chamwino Ngerengere, yeye alikamatwa akiwa na vipande vya nondo vilivyokatwa 379, na upelelezi wa mashauri hayo unakamilishwa kwa haraka ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani.
Kamanda ameongeza kuwa wamefanya jitihada mbalimbali kuzuia uhalifu katika njia ya reli kwa kushirikisha jamii kupitia mikutano mbalimbali ikiwemo ya ana kwa ana na kupitia vyombo vya habari, na kuahidi kuendelea kushirikiana na wananchi wanaotoa taarifa katika mapambano ya kuzuia vitendo vya uhalifu katika maeneo ya Reli.
Amesema katika kipindi cha mwaka jana pekee, jumla ya watuhumiwa 97 walikamatwa kwa kufanya uhalifu kwenye maeneo ya reli, na watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani na wengi tayari wamehukumiwa, hivyo kutoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa ya vitendo vya kiuhalifuili kuhakikisha mali za Shirika la Reli na miundombinu yake inakuwa salama.




