Wateja wenye madeni Tanesco watakiwa kuyalipa kwa hiyari

Msamaha wa riba watangazwa kwa watakaolipa kikamilifu
WATUMIAJI wa huduma ya umeme wenye madeni makubwa ambao wanadaiwa na Shirika la Umeme (Tanesco) wametakiwa kuyalipa madeni hayo kwa hiyari na kwamba wale watakaolipa kikamilifu watasamehewa riba.
Hayo yamebainishwa leo Juni 19, 2025 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Tanesco, Irene Gowelle wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uhamasishaji wa ulipaji wa madeni na ulinzi wa miundombinu ya umeme.
Amesema ili kuhakikisha madeni hayo yanalipwa kwa hiyari, shirika hilo limeanzisha kampeni hiyo maalum kwenye maeneo yote nchini kwa lengo la kuhamasisha ulipaji wa madeni kutoka kwa wateja wa malipo ya badaa na ukaguzi wa mita za LUKU kwa wateja wa malipo ya kabla.
Amesema zoezi hilo litaenda sambamba na kuhamasisha ulinzi wa miundombinu ya umeme, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha na kumarisha uendelevu wa upatikanaji huduma bora ya umeme kwa wananchi.
“Kampeni inaanza rasmi leo Juni 19, 2025 itakuwa endelevu na imepewa jina la “Lipa Deni, Linda Miundombinu, Tukuhudumie”, ikienda sambamba na kaulimbiu isemayo, “Huduma endelevu huanza na wewe”. Malengo ya Kampeni hii ni pamoja na kuwahamasisha wateja wa malipo ya baada kulipa madeni yao kwa hiyari kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa na kutoa motisha kwa ulipaji wa wakati ikiwemo msamaha wa riba kwa wateja watakaolipa madeni yao kikamilifu,” amesema Gowelle
Amesema misamaha ya riba itafanyika kwa kipindi cha miezi sita hivyo wateja wanaodaiwa amewataka wajitokeze kwa wingi ili kufanya mazungumzo na shirika hilo na hatimaye kulipa madeni.
Aidha Gowelle amesema zoezi hilo pia litahusisha ukaguzi wa mita za LUKU kwa lengo la kuhakikisha zinafanya kazi vizuri na hazijachezewa na wateja wasio waaminifu pamoja na kuhamasisha umuhimu wa ulinzi shirikishi wa miundombinu ya umeme kwa kuwajumuisha wananchi na kuwapa elimu ya kulinda miundombinu ya shirika.
“Miundombinu hii ndio inayowezesha upatikanaji endelevu wa huduma ya umeme kwa ufanisi hasa kwa kuzingatia kuwa ulinzi wa miundombinu ya umma ni wajibu wa kila mwananchi. Tanesco inatoa rai kwa wateja wake wote nchini ambao wanadaiwa kutoa ushirikiano kwa kulipa madeni yao kwa wakati na hivyo kutoathiri upatikanaji wa huduma ya umeme kwenye shughuli zao,” amesema
Hata hivyo Gowelle amesema Tanesco pia inatoa rai kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu vitendo vya wizi wa umeme au uharibifu na wizi wa
miundombinu ya meme kwa kushirikiana na vyombo vya dola ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza kwa ukosefu wa huduma ya umeme pamoja na kuzuia hasara kwa shirika.
Written by Janeth Jovin