Watoto wanyimwa haki ya kupata elimu ya msingi huku mzozo ukizidi Congo – UNICEF

Huku vita vikichacha na wakaazi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wakikimbia makwao, Shirika la kimataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF limetoa wito wa hatua za dharura ili kuokoa mwaka wa masomo kwa maelfu ya watoto.
Hata kabla ya mzozo huu kuongezeka, mfumo wa elimu mashariki mwa DRC ulikuwa ukikumbwa na changamoto kubwa kutokana na idadi kubwa ya wakimbizi.
Zaidi ya watu milioni 6.5, wakiwemo watoto milioni 2.6, wameathiriwa na uhamaji katika eneo hilo.
Vita kali tangu mwanzo wa mwaka zimewalazimu zaidi ya shule 2,500 kufungwa katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, pamoja na shule zilizozungukwa na wakimbizi.
Shule nyingi zimeharibiwa, na zilizosalia kubadilishwa kuwa makazi, na watoto 795,000 sasa wanakosa elimu – ongezeko kutoka 465,000 mwezi Desemba 2024 haya ni kwa mujibu wa UNICEF.
Ikiwemo mkoa wa Ituri, zaidi ya watoto milioni 1.6 mashariki mwa DRC hawana nafasi ya kusoma.
“Hii ni hali ya dharura kwa watoto,” alisema Jean Francois Basse, Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC.
Ingawa shule za Goma zilifunguliwa tarehe 9 Februari, idadi ya wanafunzi waliorejea ilikuwa ndogo, na wazazi wakisema hali ya usalama bado ni hatarishi.
Wakati mizozo inapozuka, shule zinasaidia kudumisha utulivu na kutoa ulinzi kwa watoto dhidi ya hatari za kuajiriwa na makundi ya kijeshi na unyanyasaji wa kingono.
Kulingana na UNICEF Shule pia zinatoa msaada wa kisaikolojia kwa watoto waliokutana na madhila wanapoenda kupata elimu ya msingi.
Kama sehemu ya ombi lake la misaada ya kibinadamu, UNICEF inahitaji dola milioni 52 za Marekani ili kukidhi mahitaji ya elimu ya watoto 480,000.
UNICEF pia inatoa wito kwa pande zinazohusika katika mzozo kuheshimu taasisi za elimu na mali nyingine za kiraia, kulingana na wajibu wao chini ya sheria za kimataifa. Vile vile wanajeshi wanaopigana wametakiwa kutovamia au kuendesha shughuli yoyote katika taasisi za elimu.