Habari

Watoto watatu wasikia kwa mara ya kwanza tangu wazaliwe

 

Watoto watatu waliozaliwa na changamoto ya kutokusikia, leo kwa mara ya kwanza wameanza kusikia sauti baada ya kufanyiwa upandikizaji wa kuwekewa vifaa vya kusaidia kusikia na kuwashiwa vifaa hivyo ikiwa ni mwezi mmoja baada ya upasuaji huo unaofanywa na madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Akizungumza wakati wa kuwasha vifaa hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi amesema upasuaji huu unawapa nafasi watoto hao kuweza kusikia kama watoto wengine na kuendelea na maisha ya kawaida.

“Leo tumewasha vifaa vya kusaidia kusikia kwa watoto watatu ambao walikuwa hawajawahi kusikia sauti tangu walipozaliwa, hivyo wataweza kwenda kusoma shule za kawaida kwani wana akili kama watoto wengine” amesema, Prof. Janabi

Prof. Janabi amewahimiza wazazi wenye watoto ambao wamezaliwa na hawaskii kufika hospitalini mapema ili kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa huduma stahiki kwani hadi kufikia miaka mitano watoto wanaweza kupata huduma hii na kuwapa fursa ya kuishi kama watoto wengine.

Akizungumza kabla ya kuwasha vifaa hivyo, Mtaalamu wa Mashine za zinazopandikizwa kwa watoto ili kuwasaidia kusikia Bw. Fayaz Jaffer amesema vifaa hivyo vinahitaji uangalizi wa hali ya juu hivyo amewasisitiza wazazi na ndugu wa watoto hao kuwaangalia watoto hao kwa karibu zaidi ili wasiharibu vifaa hivyo.

Ameongeza kuwa gharama za kupandikiza vifaa hivyo ni kubwa hivyo walezi wafuate maelekezo wataliyopewa na wataala
na wahakikishe wanaendelea kuwaleta katika kliniki ili kuona maendeleo yao na kufanyiwa matengenezi kinga ya vifaa hivyo kama inavyotakiwa.

Huduma ya upandikizaji vifaa hivi kwa hapa Tanzania ni TZS. 45 Mil ambapo mtoto akienda nje ya nchi ni karibu TZS. 120 Mil. Hadi sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili imepandikiza watoto 66 tangu kuanzishwa huduma hiyo hapa nchini mwaka 2017.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents