Habari

Waziri awasilisha Azimio la Mkutano Mkuu wa ILO katika Kamati ya Bunge

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amewasilisha azimio la kujumuisha suala la Usalama na Afya

Mahali pa Kazi katika misingi minne ya awali ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ya haki katika maeneo ya kazi katika vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria vinavyoendelea jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akiwasilisha azimio la kujumuisha suala la Usalama na Afya Mahali pa Kazi katika misingi minne ya awali ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) ya haki katika maeneo ya kazi katika vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria vinavyoendelea jijini Dodoma.

Azimio hilo lilipitishwa na kwa kauli moja na Nchi Wanachama wa ILO (Tanzania ikiwemo) katika Mkutano Mkuu wa 110 wa Shirika la Kazi Duniani uliofanyika Geneva, Uswisi kuanzia tarehe 27 Mei hadi tarehe 11 Juni, 2022 ambapo Waziri Mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi, Prof. Ndalichako alihudhuria akiwa ameambatana na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda pamoja na watendaji wengine wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akijibu baadhi ya hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria katika kikao cha Kamati hiyo ambacho Waziri Mwenye Dhamana ya Masuala ya Kazi, Prof. Ndalichako, aliwasilisha azimio la ILO ambalo suala la Usalama na Afya Mahali pa Kazi lilijumuishwa katika misingi minne ya awali ya Shirika hilo ya haki katika maeneo ya
kazi.

Misingi ya awali ya ILO ya haki mahali pa kazi ni pamoja na; Uhuru wa kujumuika na utambuzi wa haki ya majadiliano ya pamoja (freedom of association and the effective recognition of the right to collective bargaining), Kukomesha mifumo yote ya kazi za kushurutishwa na kulazimishwa (the elimination of all forms of forced or compulsory labour), Kukomesha ajira za watoto (the effective abolition of child labour), na Kukomesha kwa ubaguzi kwenye ajira na mahali pa kazi (the elimination of discrimination in respect of employment and occupation).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (wakwanza kushoto) pamoja na wajumbe Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakifuatilia mada ya mafunzo ya huduma ya kwanza yaliyotolewa na OSHA kwa wajumbe wa Kamati hiyo.

Kwa mujibu wa azimio hilo lililopitishwa mwaka jana, suala la usalama na afya mahali pa kazi (a safe and healthy working environment) unakuwa ni msingi wa tano wa haki katika maeneo ya kazi.

Akiwasilisha azimio hilo mbele ya Kamati ya Katiba na Sheria, Waziri Ndalichako, amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu imeona ni muhimu kuishirikisha Kamati kuhusu azimio hilo ili kuiwezesha kuyafahamu mabadiliko hayo na hivyo kuendelea kutekeleza jukumu lake la kuishauri Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi ya OSHA ipasavyo hususan katika masuala Usalama na Afya nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (wakwanza kushoto) pamoja na wajumbe Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakifuatilia mada ya mafunzo ya huduma ya kwanza yaliyotolewa na OSHA kwa wajumbe wa Kamati hiyo.

“Waheshimiwa wabunge tumeona ni vema tukawasilisha kwenu azimio hili ambalo limepitishwa na Nchi Wanachama wa Shirika la Kazi Duniani na nchi yetu ikiwemo hivyo kutokana na azimio hili masuala ya Usalama na Afya mahala pa kazi yanakuwa si wajibu wa Kisheria pekee bali haki ya msingi mahali pa kazi,” Waziri
Ndalichako ameieleza Kamati ya Katiba na Sheria.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Joseph Mhagama, amemshukuru Waziri Ndalichako kwa jitihada anazofanya katika kuhakikisha kwamba Kamati hiyo inawezeshwa kutekeleza jukumu lake la kuisimamia Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi chini yake kupitia semina na mafunzo
mbali mbali ambayo amekuwa akiyaandaa kupitia Taasisi anazoziongoza.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Joseph Mhagama (kushoto) akifuatilia wasilisho la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, katika kikao cha Kamati hiyo.

Nae Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, ameishukuru Kamati kwa miongozo na ushauri ambao imekuwa ikiitoa katika kuendelea kuboresha masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi ambapo ameahidi Taasisi yake kuendelea kufanya kazi kwa bidii pamoja na kutekeleza maelekezo na kufanyia kazi ushauri ambao umekuwa
ukitolewa na Kamati hiyo.

Wasilisho hilo la Waziri Ndalichako katika Kamati, limefanyika sambamba na mafunzo ya huduma ya kwanza mahali pa kazi ambapo wabunge hao wamefundishwa kwa vitendo namna ya kuwahudumia wafanyakazi wanaopata
changamoto mbali mbali za kiafya mahali pa kazi ikiwemo kupoteza fahamu, kuumia, kupata athari za sumu na kemikali.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (mwenye suti nyeusi), akiwa na baadhi ya watendaji katika Ofisi yake wakifuatilia wasilisho la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, kuhusu azimio lililopitishwa na Nchi Wanachama wa Shirika la Kazi Duniani katika Mkutano
wa 110 uliofanyika Geneva Uswisi Juni mwaka jana.

OSHA ni Taasisi ya Serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) wenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003. Sheria hii pamoja na mambo mengine inawataka waajiri wote kuhakikisha kwamba maeneo yao ya kazi yanatambulika na OSHA ili kufikishiwa huduma muhimu ukiwemo ukaguzi wa usalama na afya, ushauri wa kitaalam pamoja mafunzo muhimu ya usalama na afya mahali pa kazi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents