Habari

Waziri Makamba atoa maagizo mazito kwa wakandarasi

Waziri wa Nishati, Mh. Januari Makamba amesema Serikali iko katika mchakato wa kubadilisha utaratibu mzima wa kutoa kazi kwa Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kwa kuzingatia zaidi watakaokidhi vigezo vya utekelezaji miradi kwa wakati na viwango.

Waziri Makamba ameyasema hayo Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini (REA).

Waziri Makamba amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi hiyo hivyo haiwezi kukubali kuona Wananchi wakiendelea kulalamika kutokana na kucheleweshwa kwa miradi husika.

“Tuko katika mchakato wa kubadilisha kabisa namna nzima tunawapa kazi, namna nzima tunatathmini hizi kazi na mwishowe hatima yenu kama Wakandarasi wa miradi ya REA.”

Akieleza zaidi, Waziri amesema Wizara kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) itafuata taratibu zote na kuhakikisha inawaengua ambao wanasababisha malalamiko.

Aidha, amesisitiza kuwa kwa wale ambao wana utekelezaji duni zaidi na hawabadiliki, Serikali siyo tu kwamba itawachukulia hatua za kimkataba lakini pia itawashtaki kwenye Bodi ya Usajili wa Wahandisi (Contractors Registration Board) ili waondolewe katika orodha ya Wakandarasi wa Tanzania.

Waziri Makamba amesisitiza kuwa ni kwa sababu hiyo, utaratibu unabadilishwa na kwamba Mkandarasi akipewa kipande kidogo cha kazi, akikamilisha atapewa kipande kingine na siyo vinginevyo.

Kufuatia kusuasua kwa baadhi ya wakandarasi katika utekelezaji wa miradi, Waziri Makamba ametoa muda wa miezi miwili kuanzia sasa ili waitumie kurekebisha dosari na mapungufu yao ili wafikie kiwango kinachotakiwa.

“Kama ulikuwa umesuasua, uko nafasi za chini au ya mwisho, tumia muda huo wa miezi miwili kuchakarika ili ufike kwenye nafasi inayotakiwa,” ameelekeza.

Pamoja na kutoa maelekezo hayo, Waziri ameweka bayana kuwa lengo la Serikali ni kuwapa fursa wakandarasi wazawa lakini akatoa angalizo endapo wakishindwa kutimiza vigezo, basi Serikali haitasita kuwapatia kazi hizo Wakandarasi wa kimataifa waliothibitika kufanya kazi nzuri katika nchi mbalimbali.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wataalamu kutoka REA, TANESCO na Wizarani.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents