Habari

Waziri Masauni awajulia hali askari wawili walioungua ajali ya moto Mlandizi

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amewajulia hali askari wawili wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji waliojeruhiwa wakati wakiwa katika harakati za kuokoa majeruhi waliokuwa kwenye magari matatu yaliyowaka moto baada ajali kutokea eneo la Mlandizi mkoani Pwani.

Askari hao ambao wamejuliwa hali na Waziri Masauni ni 3463 Koplo Hamisi Kungwi ambaye yupo Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) na 3384 Koplo Elias Bwire yupo wodi ya kawaida, wote wapo katika Hospitali Taifa ya Muhimbili Mloganzila jijini Dar es Salaam wakiendelea kupatiwa matibabu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo mara baada ya kuwajulia hali askari hao, Waziri Masauni amesema amefika katika hospitali ya Mloganzila kwa lengo la kuwajulia hali askari hao ambao amekuwa akifuatilia taarifa zao kwa ukaribu tangu walipookolewa na kulazwa katika hospitali hiyo.

“Niliyòyasikia na kuyaona ni zaidi ya matarajio, nimekuja nakujionea mwenyewe jinsi ambavyo afya za askari hawa zinavyoendelea kuimarika, kiukweli huduma na mazingira ya hospitali ni mazuri sana, tunazidi kuwaombea ili afya zao ziendelee kuwa nzuri na hatimaye warudi nyumbani kuungana na familia zao,” amesema Waziri Masauni

Aidha amesema serikali inaendelea kuliangalia eneo la uwekeza katika mafunzo ili kuwasaidia askari wanapotekeleza majukumu yao wawe na uelewa mkubwa zaidi.

Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila, Dk. Julieth Magandi amesema askari hao anaendelea vizuri na matibabu katika hospitali hiyo.

“Sisi madaktari tunatibu ila Mwenyezi Mungu anaponya hivyo tunaendelea kuwaombea ili waweze kupata nafuu ya haraka na afya njema wapone ili watoke hospitali waendelee na majukumu yao ya kawaida.

“Tunamshukuru Rais kwa namna ambavyo Serikali yake imewekeza kwa lengo la kuhakikisha huduma zinatolewa,sisi tuna ahidi tutaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kama serikali inavyotutaka tufanye,” amesema Dk. Magandi

Kwa upande wa askari ambaye amèlazwa hospitali hapo, Koplo Bwire amesema anamshukuru Waziri na serikali kwa ujumla kwa kuweza kuwajulia hali na kuwapa mkono wa pole.

“Hii ni ajali kama zilivyoajali nyingine, ni kweli tumepata ajali tukiwa kazini lakini tunashukuru kwa namna ambavyo tumepata huduma, nakushukuru sana Waziri wa kufika hospitali hapa na kutujulia hali Mungu akubariki sana,” amesema Bwire

Ajali iliyosababisha askari hao kujeruhiwa ilitokea Machi 28 mwaka huu saa 10:15 alfajiri katika bonde la Ruvu Wilaya ya Kipolisi Mlandizi, Mkoa wa Pwani barabara ya Morogoro, Dar es Salaam.

Inaelezwa kuwa gari namba T668 DTF aina ya Scania Kampuni ya Sauli ikiendeshwa na dereva Idd Aloyce (35), mkazi wa Mafinga ikitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya liligonga ubavuni lori la mafuta ya Petroli lenye namba za usajiri RAF672N na tela lenye namban RL2594 aina ya Howo lililokuwa linatoka Dar es Salaam kwenda nchini Rwanda likiendeshwa na dereva Mushimana Musiyimana lililokuwa limesimama kupisha gari lililokuwa linakuja mbele yake.

Aidha basi hilo lilikuwa limeongozana na basi la Golden Deer Kampuni ya New Force lenye namba za usajiri RAF672N na likiendeshwa na dereva aitwaye Burton Jacob (33),.mkazi wa Mbeya ambapo nalo lililigonga kwa nyuma basi la Saul lililokuwa mbele yake na kusababisha vifo vya watu wawili ambao hawakufahamika majina yao na majeruhi watatu ambao ni Salimu Daud (50) mkazi wa Mbozi Mbeya, Farida Idrisa (26)mkazi wa Tabata Dar es Salaam na Kiambile Geofrey mkazi wa Uyole Mbeya.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents