Habari

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Serikali kuja na kifurushi cha gesi ya kupikia

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Serikali inakamilisha utaratibu wa kumruhusu mteja kuinunua kwa bei ndogo kulingana na mahitaji yake.

Kwa sasa, waziri huyo amesema wananchi wengi wanashindwa kumudu kutokana na gharama kubwa zilizopo, hivyo mchakato wa kuzipunguza unaelekea mwishoni ili kulifanyia mapinduzi suala hilo.

“Moja ya vikwazo kwa Watanzania kutumia gesi ni kwamba lazima uwe na fedha nyingi kwa mkupuo. Teknolojia inayoruhusu mtu kununua gesi ya Sh500 au Sh 1,000 ipo. Baada ya muda tutaileta sokoni ili watu waanze kununua gesi kama wanavyonunua kopo la mkaa au fungu la kuni,” alisema Makamba.

Waziri huyo alibainisha mpango huo alipofanya mahojiano na Mwananchi, ofisini kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni kuzungumzia masuala mbalimbali ikiwa siku chache baada ya kuhitimisha ziara aliyoifanya katika mikoa ya Mara, Mwanza, Tabora, Shinyanga, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, Simiyu, Geita na Kagera.

Ziara hiyo ililenga kukagua shughuli zinazotekelezwa na taasisi zilizopo chini ya wizara yake ukiwamo Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).

Kwa sasa gesi inayouzwa kwa mtungi wa kuanzia kilo sita, ni wastani wa Sh25,000 hivyo kuwa juu ya mahitaji ya baadhi ya wanaohitaji kiasi kidogo kwa matumizi yao au wasio na uwezo wa kifedha kumudu bei ya mtungi huo.

“Teknolojia hiyo itakuwa mkombozi kwa Watanzania na itapunguza matumizi ya kuni na mkaa kupikia hasa kwa wananchi wa vijijini. Mazingira yetu yanafanana na India kwa kiasi kikubwa lakini wao asilimia 98 wanapika kwa kutumia gesi,” alisema Makamba.

Makamba alisema kiuhalisia bei ya gesi ni rahisi kuliko mkaa na kuni, lakini wananchi wamezoea kununua kuni na mkaa katika vipande vidogovidogo ndio maana haionekani kuwaumiza wengi hivyo gesi inahitaji ubunifu wa kibiashara ili kuendana na uwezo na mahitaji ya Watanzania.

Katika kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo salama, Makamba alisema Serikali imeondoa kodi kwenye mitungi ya gesi hiyo inayotengenezwa nchini ili bei yake iwe rahisi kwa wengi kuimudu.

Matumizi ya kuni na mkaa, alisema yana madhara mengi ya kiafya na takwimu za Wizara ya Afya za mwaka 2017, zinaonyesha watu 22,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa hewa yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na matumizi ya nishati hiyo.

“Bila kujali mtu anaishi mjini au kijijini, lazima atakuwa na jiko, liwe limejengwa au amepanga mafiga tu nje ya nyumba. Matumizi ya kuni kwenye kupika kwa saa tu ni sawa na kuvuta sigara 300. Kupika ni miongoni mwa mambo yanayotuunganisha na vijijini, wanawake wanatumia muda mrefu kutafuta kuni,” alisema.

Ili kubadilisha nishati ya kupikia, Makamba alisema ameshapatikana mshauri elekezi anayeandaa mpango wa kuongeza matumizi ya nishati jadidifu (biogas) ambao utakamilika Desemba mwaka huu.

Vilevile, alisema wizara hiyo imeandaa maonyesho ya kupika yanayolenga kuongeza ubunifu na kubadilishana uzoefu wa kuandaa chakula kwa gharama nafuu na nishati salama. Kwenye ziara aliyoifanya mikoani, Makamba alionekana akigawa mitungi ya gesi ya kupikia suala alilolielezea kuwa ni sehemu ya utafiti ambao wizara inafanya kujua uwezo wa wananchi wa vijijini kumudu nishati hiyo.

“Tunafuatilia kuona ni wangapi wataendelea kuitumia mitungi ile. Ni taarifa muhimu ambazo wizara inazihitaji kwa ajili ya kuweka mikakati ya kitaifa,” alisema.

Alisema Serikali lazima itengeneze mipango kutokana na ushahidi ilioukusanya kutoka kwa wananchi inaowahudumia.

“Tunataka tujue wanaitumiaje, ingawa asilimia 50 ya wanaopewa bure mitungi wanaendelea kuitumia. Bibi tuliyempa mtungi kijijini asipouwasha na kuutumia au asipoendelea kuutumia baada ya kumaliza gesi aliyopewa ni taarifa muhimu kwetu. Septemba au Oktoba mwaka huu tutafanya mkutano mkubwa nchini kuhusu kupika,” alisema.

Ukiacha wananchi waliopewa mitungi hiyo, Makamba alisema Serikali imekipa Chuo cha Uuguzi Peramiho mtungi wa tani moja wa gesi ya kupikia, ili kujifunza kabla ya kupitisha mwongozo utakaozitaka taasisi zote zinazopika chakula cha kuanzia watu 300 kutumia gesi asilia. “Serikali imetenga Sh10.5 bilioni mwaka huu ili kuhamasisha matumizi ya gesi maeneo ya mijini. Huu ni mpango unaolenga kuhama kutoka kutumia kuni na mkaa kwenda kwenye gesi. Mwanzo mwelekeo ulikuwa viwandani na wenye magari lakini sasa hivi tunaipeleka katika kupika,” alisema.

Gesi kwenye magari

Ukiacha kupika, Makamba alieleza mkakati wa kuongeza matumizi ya gesi asilia kwenye magari ili kukabiliana na ongezeko la bei ya mafuta inayoendelea kupanda kila siku.

Alisema kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo, sekta binafsi inashirikishwa ili kufanikisha ujenzi wa vituo vingi vitakavyotumika kujaza gesi hiyo mikoani hivyo kuwaruhusu madereva kuipata mahali popote watakapokuwepo nje ya Dar es Salaam ambako kuna vituo viwili mpaka hivi sasa.

Ukiacha mpango huo, alisema hamasa hiyo inafanywa serikalini pia ili magari ya taasisi nyingi za umma yaanze kuitumia nishati hiyo salama. Takwimu zinaonyesha matumizi ya mafuta kwenye magari yanachangia kuzalisha asilimia 40 ya hewa ya ukaa, ndio maana kampuni za magari zimepanga kuachana nayo ifikapo mwaka 2050.

“Tumezungumza na uongozi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) kwamba mabasi yao mapya 300 yatakayotumika katika njia mpya, yatumie gesi badala ya mafuta. Mabasi haya yapo Dar es Salaam hivyo ni rahisi kupata gesi. Haya yatatoa picha ya kufunga mfumo huo kwenye magari mengi ya taasisi nyingine,” alisema.

Ingawa idadi ya wanaotaka kufunga mfumo wa gesi kwenye magari yao inazidi kuongezeka, changamoto iliyopo ni gharama kubwa zilizopo kwani huanzia Sh2 milioni mpaka takriban Sh4 milioni kutokana na ushuru wa forodha wa vya vifaa muhimu vinavyounda mfumo huo.

Kuhusu uwezekano wa kuviondolea kodi vifaa hivyo ili kushusha gharama za mfumo, Makamba alisema: “Hilo sio suala letu. Kodi inasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango, ila a tutazungumza nao kuona uwezekano wa kutoa unafuu huo.”

Uunganishaji umeme

Siku za hivi karibuni wananchi wamekuwa wakilalamika kuchelewa kuunganishiwa umeme hata baada ya kulipia gharama zote muhimu hivyo kulazimika kuendelea.

Kuhusu ucheleweshaji huo uliojitoeza katika maeneo mengi nchini, Makamba alisema wakati anaingia katika wizara hiyo baada ya kuteuliwa Septemba mwaka jana alikuta kuna zaidi ya maombi 140,000 ya wateja wanaoubiri kuunganishiwa umeme. Alisema tatizo lililosababisha hali hiyo lilikuwa kuchelewa kwa baadhi ya vifaa muhimu vinavyoingizwa kutoa nje ya nchi.

Hata hivyo, kwa taribani mwaka mmoja sasa alisema juhudi kubwa zimeelekezwa huo na wengi wameunganishwa isipokuwa 30,000 ambao mpaka mwishoni mwa mwezi huu watakuwa wameshapata huduma hiyo.

“Transfoma na nyaya za copper (shaba) na aluminium ndizo zilikuwa adimu. Tumelishughulikia hilo na kila meneja wa Tanesco ameahidi kupeleka umeme kwa wateja wanaosubiri ndani ya mwezi huu. Tulinunua vifaa vingi kwa mpigo na kuvisambaza mikoani kote,” alisema Makamba.

Kuhusu makandarasi waliopewa kazi kutokuwapo katika vijiji walivyopangiwa, alisema aligundua sababu tatu zilizowafanya makandarasi hao wa REA kuchelewesha miradi.

“Wapo waliohamishwa maeneo kwa maelekezo maalumu hivyo kukosa fedha za kurudi mahali walikotakiwa kujenga mradi husika, lakini kupanda kwa bei ya copper na aluminium kuliwaumiza baadhi yao,” alisema Makamba.

Kutokana na sababu tofauti, alisema baadhi ya makandarasi walifilisika kiasi cha kushindwa kabisa kuendelea na kazi waliyopewa lakini hayo yote kwa sasa, alisema yameshughulikiwa ipasavyo.

Umeme endelevu

Ili kuwa na umeme endelevu, waziri alisema mkakati uliopo ni kuongeza vyanzo mbadala badala ya kuendelea kutegemea zaidi maji na gesi asilia kwani Tanzania inazo rasilimali nyingi zinazofaa kuzalisha umeme.

Rasilimali hizo alizitaja kuwa ni makaa ya mawe, maporomoko ya maji, upepo, jotoardhi, jua, gesi na hata mabaki ya mimea na wanyama (biogas).

“Lengo la kwanza ni kuchanganya vyanzo vya kuzalisha umeme utakaoingia katika gridi ya Taifa. Serikali imeamua kwenda na vyanzo vyote safari hii,” alisema Makamba.

Ni kutokana na umuhimu huo alisema Tanesco imeingia mkataba na kampuni ya Masdar ambayo ni ya Serikali ya Falme za Kiarabu (UAE) kuzalisha megawati 2,000 za nishati jadidifu.

“Umeme huu utakuwa nafuu. Mkataba wake ni sehemu ya makubaliano ya kiserikali yaliyofanyika wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara nchini humo hivi karibuni,” alisema.

Umeme visiwani, mafuta vijijini

Kwenye ziara aliyoifanya katika baadhi ya mikoa, Makamba alisema amegundua kuna mahitaji makubwa ya umeme nchini hasa vijijini kwenye maeneo yaliyochangamka pamoja na yale yenye shughuli za uzalishaji.

Ukiacha maeneo hayo, alisema migodini, machimboni na visiwani ni maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa wa nishati, ambayo mikakati imeshawekwa kuhakikisha inafika ili itumiwe na wananchi walioko huko.

“Tumejipanga kupeleka umeme kwenye kila mgodi, uwe mkubwa au mdogo na katika maeneo yote yenye uzalishaji wa mashine mbili za kusaga nafaka.

Sasa hivi tunapeleka umeme katika visiwa 47 kwa mpigo katika Bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Tanganyika na Ziwa Nyasa. Tumeamua kuja na vitu vipya katika bajeti vinavyogusa maisha ya Watanzania,” alisema Makamba.

Ukiacha jitihada za kupeleka umeme zinazoendelea, Makamba alisema wananchi wengi hasa wa vijijini wanatumia mafuta machafu kutokana na changamoto zilizopo xa kuyasafirisha kutoka mjini na kuyahifadhi, suala ambao wizara inalishughulikia kwa kipaumbele kikubwa.

Kati ya changamto zilizokuwa zinazuia ujenzi wa vituo hivyo maeneo ya vijijini, ni masharti ya Ewura yanayoweka vipimo vya urefu na kina cha tanki, nguzo za kituo, paa hata zege litakalomwaga ambavyo gharama yake ni Sh300 milioni.

“Tulichofanya sasa hivi ni kulegeza masharti. Tumejiridhisha kuwa kijijini inawezekana kujenga kituo kwa Sh40 milioni.

Tunafahamu wajasiriamali wengi vijijini hawana mtaji wa kutosha, Serikali imetenga Sh2 bilioni kwa ajili ya kuwakopesha, tukipata mafanikio mwaka huu, mwakani tutaweka fedha nyingi zaidi,” alisema Makamba.

Wanaotaka kunufaika na fedha hizo alisema wameanza kujitokeza kuomba ila wizara imezielekeza halmashauri kuhakikisha wanaonufaika nazo ni wakazi wa vijijini kweli ili wasije wakajitokeza wajanja wachache wanaojikujinufaika nazo.

Kwa wafanyabiashara wenye mtaji mkubwa, alisema hawatoruhusiwa kunufaika na mkopo huo isipokuwa watalegezewa masharti ya kujenga vituo vijijini.

 

Chanzo Mwananchi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents