Wazungu watatu wakamatwa kwa kupanga kushambulia misikiti na masinagogi Uingereza

Waingereza watatu wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia walipanga kukusanya silaha, ikiwa ni pamoja na bunduki, ili kutekeleza shambulio kama sehemu ya vita dhidi ya wasiokuwa Wazungu, wamesema waendesha mashtaka siku ya Jumatano.
Brogan Stewart na Marco Pitzettu, wote 25, na Christopher Ringrose, 34, wanadaiwa kupanga kitendo cha kigaidi, kulenga misikiti au masinagogi, walipokamatwa Februari 2024.
Watatu hao pia wanashtakiwa kwa makosa mawili ya kukusanya taarifa ambazo zinaweza kuwa na manufaa kwa mtu anayetayarisha kitendo cha kigaidi.
Wamekana makosa na wanaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Sheffield, ambapo mwendesha mashtaka Jonathan Sandiford amesema washtakiwa watatu “wana itikadi kali za mrengo wa kulia na wanajiona kuwa ni wanasoshalisti au Wanazi.”
Sandiford amesema watatu hao walionyesha kumpenda Adolf Hitler na kuwahusudu wahusika wa mashambulizi ya kigaidi, pamoja na chuki kwa watu wasiokuwa weupe, hasa Waislamu na wahamiaji.
“Imani yao ni kwamba lazima hivi karibuni kutakuwa na vita kati ya Wazungu ana jamii nyingine,” aliongeza Sandiford.
Miongoni mwa mamia ya jumbe zao, Stewart alichapisha swali kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram akiuliza “tunamuuaje waziri mkuu,” ambaye wakati huo alikuwa Rishi Sunak.
Katika kundi la Facebook, Stewart alisema: “Kuna haja ya kuwasha moto kwenye vyumba vya gesi na kuondoa uchafu katika nchi hii. Ifanye Uingereza kuwa nzuri tena.”
Washtakiwa waliunda kundi la Telegram liitwalo “Einsatz 14” mwezi Januari 2024, ambalo Sandiford alisema lilikuwa “kundi la kuchukua hatua badala ya maneno.”
Wanachama wengine watatu wa kundi hilo walikuwa ni maafisa wa siri polisi, amesema mwendesha mashtaka.




