Wizara ya Maji yazindua mpango wa Bilioni 94.7 kuimarisha huduma za maji Hanang’

Wizara ya Maji imezindua mpango maalum wa uwekezaji wa maji safi, usafi wa mazingira na usafi binafsi wenye thamani ya Sh bilioni 94.62 wilayani Hanang’, mkoani Manyara.
Mpango huo wa miaka mitano wa Shirika la WaterAid Tanzania umezinduliwa Februari 11, 2026 na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ukiwa na lengo la kutatua changamoto ya ukosefu wa maji katika vijiji vya wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Naibu Waziri amesema rasilimali zinazotarajiwa kupatikana kupitia vyanzo vya kawaida hadi mwaka 2030 ni Sh bilioni 41.75 pekee, hali inayoacha pengo kubwa la kifedha.
Amesema mchango wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo, huku akitoa wito kwa wadau kuhakikisha mpango huo unaingizwa kikamilifu katika mipango na bajeti za kila mwaka.
“Wadau wa maendeleo na sekta binafsi wauone mpango huu kama ramani na mwaliko rasmi wa kuwekeza Hanang’,” amesema Mhandisi Mathew.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Hanang’, Almish Hazal, amesema pamoja na jitihada za ujenzi wa visima, changamoto kubwa ni upatikanaji wa nishati ya uhakika. Ameomba ushirikiano kati ya Tanesco na RUWASA ili kuimarisha huduma za umeme kwenye miradi ya maji.
“Tutakapopata umeme wa uhakika, tutakuwa tumemtua mama ndoo kichwani kwa asilimia 100,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga, ameipongeza Serikali kwa ushirikiano wake na kuomba kipaumbele zaidi katika rasilimali za utekelezaji wa mpango huo.
“Tunatoa mwaliko wa wazi kwa wadau wote kushiriki. Serikali iendelee kuongoza kwa kutoa kipaumbele cha uwekezaji, na sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo waunge mkono juhudi hizi,” amesema.
Written by Walter





