
China imethibitisha leo kuwa kiongozi wa nchi hiyo Xi Jinping atakutana na mwenzake wa Marekani Joe Biden wiki inayokuja pembezoni mwa mkutano wa kilele wa kundi la mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi la G20 utakaofanyika nchini Indonesia.
Taarifa hiyo imetolewa na msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa China ambaye pia amearifu kwamba rais Xi atakuwa na mazungumzo na viongozi wengine ikiwemo wa Ufaransa, Senegal na Argentina.
Ikulu ya Marekani tayari ilithibitisha hapo jana kuwa rais Biden atakutana na Xi Jumatatu inayokuja kwa mazungumzo yao ya kwanza ya ana kwa ana tangu Biden alipochaguliwa kuwa rais wa Marekani.
Washington imesema mazungumzo hayo yatagusia njia za kuimarisha ushirikiano kati ya China na Marekani pamoja na kuyatafutia majibu masuala yanayotatiza mahusiano baina ya madola hayo mawili ikiwemo hadhi ya kisiwa cha Taiwan.