Michezo

Yanayosubiriwa Uzinduzi wa Uwanja wa Singida

LEO Jumatatu, Machi 24, 2025, ni siku ya kihistoria kwa wapenda soka wa Mkoa wa Singida na taifa kwa ujumla, kwani klabu ya Singida Black Stars inazindua rasmi uwanja wake mpya. Uzinduzi huu ni hatua kubwa kwa klabu hiyo, ambayo imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo ili kuinua kiwango cha soka nchini.

.
Uwanja huo uliopo Mtipa mkoani Singida, umejengwa kwa viwango vya kisasa ukiwa na nyasi bandia kwa kushirikiana na wadhamini wakuu wakiwamo Airtel, Azam, GSM. NBC, SBS, na MO Dewji. Uwanja huu una uwezo wa kuchukua mashabiki 5,000 hadi 7,000 na unatarajiwa kuwa kitovu cha mashindano makubwa ya kitaifa na kimataifa.

Sherehe za uzinduzi zinatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na michezo, huku mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA. Aidha, viongozi wa TFF nao wanatarajiwa kushiriki.


.
Burudani mbalimbali zimetayarishwa kabla ya mechi kuu, ikiwa ni pamoja na muziki kutoka kwa wasanii maarufu wa Bongo Fleva, michezo ya asili, na maonesho ya utamaduni wa Kisingida. Mashabiki watapata fursa ya kushuhudia historia ikiandikwa kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huu mpya.

 

.
Kilele cha tukio hili kitakuwa ni mchezo wa kirafiki kati ya wana familia wawili Singida Black Stars na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania, Yanga SC utakaochezwa kuanzia saa 10 jioni. Mechi hii inatajwa kuwa ya kuvutia kutokana na nafasi za timu hizi katika msimamo wa ligi, ambapo Yanga wanaongoza kwa pointi 58 huku Singida Black Stars wakiwa nafasi ya nne na pointi 44.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents