Yanga ni sawa na Mamelodi Sundowns – Edo Kumwembe

“HATUJUI sana mbele ya safari, lakini wote tuliona namna ambavyo Kaizer Chiefs waliteketea mbele ya Yanga katika dimba la Bloemfontein pale Afrika Kusini. Kilikuwa kichapo kikali mbele ya mashabiki wao. Mabao 0-4. Kuna mambo ambayo tunaweza kuchukua peni na kuandika.
Kwanza Kaizer Chiefs wamewekwa katika nafasi yao na Yanga. Kwamba kwa sasa Yanga wapo katika hadhi ya kina Mamelodi Sundowns na sio tena Kaizer Chiefs na Orlando Pirates. Hawa Mamelodi wamewekeza pesa nyingi kiasi cha kuziacha nyuma Orlando Pirates na Kaizer Chiefs.
Yanga na Simba sasa hivi wanatamani kuwa kule juu. Dalili kwa Yanga zilianza kujionyesha wakati bao la Aziz Ki lilipokataliwa pale Pretoria. Yanga walikuwa wanaitoa Mamelodi katika pambano lile na wangeweza kusonga mbele. Hapo Yanga walikuwa wanajiweka katika hadhi ya Mamelodi. Kama unaweza kupambana na Mamelodi kwanini usiiadhibu Kaizer Chiefs ambayo msimu uliopita ilishika nafasi ya 10 katika Ligi Kuu Afrika Kusini.
Labda wanaweza kurudi tena siku za usoni, lakini kwa sasa Kaizer wapo chini ya Yanga. Sijawatazama vyema watani zao Orlando Pirates, lakini kwa nilichokiona juzi, Nasreddine Nabi na mabosi wa Kaizer wanapaswa kufahamu kwamba kuna timu kutoka Afrika Mashariki ipo juu yao kwa sasa. Hata mashabiki wa Kaizer wameshuhudia hivyo.”