
Ligi Kuu inarudi kuanzia leo baada ya awali kusimama tangu Disemba 29 kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) ambazo zilikuwa zianze leo Februari Mosi hadi Februari 28 kabla ya kuahirishwa hadi Agosti mwaka huu.
.
Mechi ya kwanza ya kiporo cha ligi inachezwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, wakati Yanga itakapoikaribisha Kagera Sugar. Hesabu kwa Wananchi ni kuhakikisha wanaondoka na pointi tatu, lakini kubwa ni vita ya ubingwa ambao inaanza rasmi kuanzia kwenye ngwe hii ya lalasalama.
.
Ushindi wa Yanga una maana ya kuirudisha kileleni na kuiengua Simba, kwani timu hizo mbili zinatenganishwa kwa tofauti ya pointi moja tu kwa sasa, Wekundu wakiwa na pointi 40 moja zaidi ya ilizonazo Yanga yenye 39 licha ya kila moja kucheza mechi 15.
Kagera yenyewe ni kama inapigania roho yake ikiwa nafasi ya 15 chini kabisa mwa msimamo na kwenye rekodi zinawakataa mbele ya wapinzani wao hao kwani katika mechi 10 zilizopita baina yao katika Ligi Kuu, haijawahi kupata ushindi wowote zaidi ya kuambulia sare mbili na kupoteza michezo mingine minane iliyosalia ukiwamo wa msimu huu walipolala mabao 2-0 Kaitaba, Bukoba.