Habari

Zaidi ya watu 300 wafariki Dunia katika tetemeko la ardhi Haiti

Watu zaidi ya 300 wamefariki dunia nchini Haiti baada ya nchi hiyo ya Carrebean kukumbwa na tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.2 liliporomosha majumba na miundombinu kadhaa.
Haiti | Erdbeben auf Haiti | Zerstörung
Tetemeko hilo liliitikisa eneo la kusini mwa nchi hiyo siku ya Jumamosi (Agosti 14) na, kulingana na idara ya ulinzi wa raia ya Haiti, watu wengine zaidi ya 1,800 walijeruhiwa.

Nguvu za tetemeko hilo limeyageuza majengo mengi kuwa kifusi.

Waziri Mkuu wa Mpito Ariel Henry alisema nchi yake inahitaji msaada mkubwa na kwamba angelitangaza hali ya hatari kutokana na janga hilo.

Kikosi cha uokoaji na raia waliojitolea walifanikiwa kuwaokoa watu wengi kutoka kwenye vifusi na bado walikuwa wanaendelea na zoezi hilo.

Hata hivyo, ilikuwa vigumu kutathmini kiwango hasa cha uharibifu kutokana na ugumu wa kuyafikia maeneo yaliyoathiriwa.

Idara inayoshughulika na utafiti wa jiolojia nchini Marekani (USGS) ilitahadharisha kwamba idadi ya vifo kutokana na tetemeko hilo inaweza kuwa kubwa.

USGS ilisema kitovu cha maafa hayo ni eneo la Ghuba ya Haiti, lililopo takribani kilomita 125 magharibi mwa mji mkuu, Port-au-Prince.

Idara hiyo ya jiolojia ya Marekani ilibainisha kuwa makaazi mengi katika eneo hilo yamejengwa kwa matofali na ni hatari wakati linapotokea tetemeko la ardhi.

Kwa mujibu wa gazeti la Dominican Diario Libre katika nchi jirani ya Jamhuri ya Dominica, ambayo inagawana kisiwa cha Hispaniola na Haiti, mtetemeko huo ulitikisa pia eneo hilo.

Vilevile Jamaica, ambayo ipo umbali wa mamia ya kilomita kutoka Haiti pia iliripoti kutikiswa na tetemeko hilo la ardhi.

Marekani yatuma salamu za pole
Haiti | Erdbeben auf Haiti | Zerstörung

Raia wakisiaidiana kwenye uokowaji wa wahanga wa tetemeko nchini Haiti.

Rais Joe Biden wa Marekani alituma salamu za pole kwa wale wote walioathiriwa kwenye janga hilo nchini Haiti.

Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), Samantha Power, alisema wataalamu wa kushughulikia maafa wapo nchini Haiti wakichunguza uharibifu uliotokea na kutathmini mahitaji.

Annalisa Lombardo, mkurugenzi wa shirika kubwa la misaada nchini Ujerumani la Welthungerhilfe nchini Haiti, aliliambia shirika la habari la Ujerumani (dpa) kwamba alipokea habari za kutokea uharibifu mkubwa wa majengo, lakini mji mkuu wa Port-au-Prince, ambako anaishi haukuathirika sana.

Lombardo alisema shirika lake linawasiliana na mashirika mengine ya misaada kuhakikisha kuwa walioathirika wanapatiwa mahitaji muhimu kama maji, chakula na malazi.

Miongoni mwa watu waliokufa ni seneta wa zamani Jean Gabriel Fortune, aliyekufa baada kufunikwa chini ya kifusi kwenye hoteli yake iliyopo katika jiji la Les Cayes, kulingana na gazeti moja la Haiti.

Shuhuda mmoja kutoka Les Cayes, ambao ni mmoja kati ya miji mikubwa nchini Haiti, alilielezea shirika la habari la Haiti (HPN) juu ya nyumba na hoteli zingine zilizoanguka na juu ya watu waliozikwa chini ya kifusi.

Hospitali zalemewa
Erdbeben auf Haiti

Madhara ya tetemeko la ardhi nchini Haiti.

Vyombo vya habari katika eneo hilo vimesema hospitali katika maeneo yaliyoathirika zaidi zimeripoti kuelemewa katika utoaji wa huduma za dharura.

Haiti ni miongoni mwa nchi masikini zaidi ulimwenguni na bado inapambana na athari za tetemeko la ardhi lililotokea Januari 12, 2010 lililokuwa na ukubwa wa 7.0 ambapo watu 220,000 walikufa, 300,000 kujeruhiwa na watu wengine milioni moja waliachwa bila makaazi.

Uharibifu uliosababishwa na tetemeko hilo la ardhi, ambalo lilipiga kwenye eneo linalokaliwa na watu wengi katika mji mkuu wa Port-au-Prince ulikadiriwa kuwa dola bilioni 8.

USGS ilisema huenda mfumo wa tetemeko la ardhi la siku Jumamosi na ambalo pia lilisababisha matetemeko madogo ya ardhi baadaye ukawa sawa na tetemeko hilo la ardhi lililoikumba Haiti zaidi ya muongo mmoja uliopita.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents