Habari

“Zilipopigwa risasi hewani, Mbowe alikimbia mpaka miwani ikadondoka” Shahidi afunguka Mahakamani kesi ya viongozi wa CHADEMA

Ushahidi katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akiwamo Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe, uliotolewa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Gerard Rich, umedai kwamba aliamuru kikosi cha mabomu ya machozi kurudi nyuma na kile cha silaha za moto.

Kadhalika alidai kuwa kitendo cha washtakiwa kukiuka amri yake kupitia redio upepo iliyowataka kusitisha maandamano kwa mara ya pili, alilazimika kuamuru askari wenye silaha ya moto kusonga mbele.

SSP Rich ambaye pia ni Ofisa wa Polisi wa Operesheni Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, alitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimba, akisaidiana na Mawakili wa Serikali, Wankyo Simon, Jacqline Nyantori na Salim Msemo.

Akiongozwa na Nchimbi shahidi alidai kuwa Februari 16, 2018, aliitwa na bosi wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RPC), (wakati huo) ACP Jumanne Mlilo, akiwa na maofisa wenzake, walipewa maelekezo ya kazi kuimarisha ulinzi wakati wa kufunga kampeni pamoja na uchaguzi mdogo wa ubunge siku inayofuata Jimbo la Kinondoni.

Alidai vyama vyote vya siasa vilikuwa na mikutano katika viwanja tofauti jimboni humo, Chadema walikuwa viunga vya Buibui Kata ya Mwananyama, Chama Cha Mapinduzi (CCM), viunga vya Biafra, Kata ya Kinondoni, Chama cha Wananchi (CUF), viunga vya Vegas, Kata ya Makumbusho.

Alidai kuwa mkuu wa ulinzi Chadema, alikuwa SSP Dotto, CUF alikuwa Mrakibu (SP) Batseba na CCM alikuwa SP Magai na wote watatu walitoa taarifa kwake kwa njia ya simu kuhusu hali ya ulinzi.

Ilipofika saa 11:30 alipata taarifa kutoka kwa SSP Dotto kwamba katika jukwaa la Chadema, viongozi wamepanda jukwaani wametoa kauli zenye dalili ya uvunjifu wa amani ikiwamo kuhamasisha wafuasi kufanya maandamano,” alidai shahidi na kuongeza.

Hamasa iliongezeka wakazuia makutano ya barabara ya Kawawa na Mwananyamala kwa madai ya kwenda Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa Kinondoni, nilimwamuru dereva awashe king’ora, walitawanyika kutupisha, lakini walivyoona gari ya polisi walirejea kwenye barabara ya mwendo wa haraka na kusababisha magari kushindwa kuendelea na safari yake.“.

Nilitoa ilani kuwataka wasitishe maandamano hayo kwa sababu si halali, nilimwona Salum Mwalimu, akiwa kwenye gari ya wazi, Mbowe akiwa ameongozana na viongozi wengine walioko kizimbani wakihamasisha, huku wakiimba ‘haya twende Mbowe anatisha, hatupoi, hatishwi lazima tufike kwa mkurugenzi,” alidai shahidi.

Akifafanua zaidi alidai kuwa maandamano hayo yalisababishwa na wahalifu kupora kwenye maduka, watoto na wazee kukimbilia vituo vya polisi.

Alidai alitoa amri askari kuwarushia mabomu ya machozi waandamanaji, lakini upepo uliwarudia na moshi wake uliwarudia askari, wawili kati yao walianguka chini kwa kujeruhiwa akiwamo Konstebo Fikiri na Koplo Rahmu kujeruhiwa.

Nililazimika kutoa ilani kwa mara ya tatu, nikawaamuru askari wenye silaha ya moto kusonga mbele wakapiga risasi juu kuwatawanya, katika tukio hilo pia alijeruhiwa Akwirina na baadaye alivyopelekwa hospitali ya Mwananyamala alifariki,” alidai bosi huyo wa Jeshi la Polisi.

Alidai kuwa baada ya zile risasi kuanza kupigwa hewani, alimwona Mbowe akitimua mbio na kutawanyika.

Mheshimiwa nilikuwa sijui kama Mbowe anajua kukimbia alitimua mbio mpaka miwani yake ilianguka,” alidai SSP Rich.
Aidha, shahidi alidai kuwa anawatambua washtakiwa na kwamba aliwaona siku ya tukio.

Jopo la mawakili wa utetezi liliongozwa na Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala, Hekima Mwasipu, Jeremia Mtobesya na John Mallya.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili Kibatala na shahidi:

Kibatala: Je, shahidi uliwahi kufanya mahojiano na wenye maduka baada tukio na ulichukua maelezo?

Shahidi: Hapana.
Kibatala: Katika ushahidi wako umemtaja Akwilina unaweza kumtaja majina yake yote mawili?
Shahidi: Sijui.
Kibatala: Kuhusu kufyatua risasi, je, zilitumika ngapi?
Shahidi: Risasi baadhi zilienda hewani na nyingine sifahamu.
Kesi hiyo itaendelea ushahidi wa Jamhuri Mei 13, 14 na 15, mwaka huu.
Mbali ya Mbowe, wengine ni, Katibu Mkuu Taifa, Vicent Mashinji, Mbunge wa Bunda Ester Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Katibu Mkuu Taifa, Vicent Mashinji, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na John Heche.

Chanzo: GAZETI LA NIPASHE

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents