Habari

Machinga Dar kupangwa kwa utaratibu, RC Makalla azindua kitabu cha mwongozo (+ Video)

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla leo September 17 amezindua kitabu Cha mwongozo wa Mpango wa kuwapanga Machinga Dar es salaam na kutoa wito kwa Wote wanaofanya biashara Kwenye maeneo yasiyo rasmi kuanza maandalizi ya kupangwa kwenye maeneo rasmi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo RC Makalla amesema mpango huo unawalenga Wafanyabiashara waliojenga Vibanda juu ya Mifereji na mitaro ya Maji, Wanaofanya biashara mbele ya Maduka, Wanaofanya biashara Kwenye hifadhi ya Barabara, Wanaofanya biashara Kwenye njia za watembea kwa miguu na waliojenga Vibanda mbele ya Taasisi za Umma zikiwemo shule.

Ili kufanikisha Mpango huo RC Makalla ametoa maelekezo maalumu ikiwemo Kila Manispaa na TARURA kuweka Vibao vya Makatazo ya Ufanyaji biashara Kwenye maeneo yasiyo rasmi, Kila Manispaa kuweka dawati la kushughulikia kero za Machinga, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Maafisa Biashara na Viongozi wa kata na Mitaa kufanya ufuatiliaji ili Wafanyabiashara wasirudi kwenye maeneo yasiyo rasmi.

Aidha RC Makalla ametoa katazo la kuwataka Wafanyabiashara Wenye Maduka wanaopanga bidhaa zao mbele ya Maduka na kuzui njia za watembea kwa miguu kuacha Mara moja huku akiwaelekeza Wafanyabiashara, wenye nyumba na Taasisi kutoruhusu Machinga kufanya biashara kwenye njia za watembea kwa miguu.

Kwa upande wake makamu Mwenyekiti wa Machinga Bwana Steven Lusinde amesema kwa niaba ya Machinga wamepokea kwa mikono miwili Mpango huo kwakuwa umelenga kuwaboreshea mazingira Machinga na wapo tayari kwa utekelezaji ili kufanikisha Mpango huo.

Kitabu Cha Mpango wa kuwapanga Machinga Dar es salaam kimeandikwa kwa mikono ya Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Amos Makalla baada ya kufanya utafiti wa kina na kuwashirikisha Wadau na sekta mbalimbali ambapo moja ya sababu ya kukwamisha suala la Usafi ilionekana ni Ufanyaji biashara holela ambapo kupitia Mpango huo ni Imani kubwa kuwa Jiji la Dar es salaam linakwenda kuwa safi na lenye hadhi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents