Habari

Watatu wakamatwa kwa kumteka mtoto Mbeya

Jeshi la Polisi limesema limefanikiwa kumpata mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 05 mwanafunzi wa Shule ya awali Isaiah Samartan iliyopo jijini Mbeya aliyeripotiwa kupotea mei 15,2024 muda wa saa 11:45 jioni huku Jeshi hilo likiwashikilia watuhumiwa watatu kuhusiana na tukio hilo.

Akitoa taarifa hiyo Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime amesema
tukio hilo liliripotiwa na Baba mzazi wa mtoto aitwaye Layson Mkongwi, Mfakanyakazi wa Kampuni binafsi huko Jijini Mbeya ambaye alipokea simu kutoka kwa mtu asiyefahamika na kumweleza kuwa hatampata mtoto wake hadi atakapomtumia kiasi cha shilingi milioni ishirini (20,000,000=).

Ameongeza kuwa Jeshi hilo baada ya kupokea taarifa hizo lilianza uchunguzi na kufanikisha kupatikana kwa mtoto huyo akiwa salama Pamoja na mtuhumiwa ambae ni Winfred Martin Komba, miaka 36, Mkazi wa Vingunguti Dar es Salaam ambaye ndiye aliyekuwa akimpigia simu baba mzazi wa mtoto na kumtishia atoe fedha.

Watuhumiwa wengine waliokamatwa ni Mama mzazi wa huyo mtoto aitwaye Agnes Jacob Mwalubuli mkazi wa Isyesye Mbeya ambaye alipanga njama na mtuhumiwa ili kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Baba mzazi wa mtoto huyo.

Mtuhumiwa Wilfred Komba baada ya kuhojiwa alieleza kuwa baada kupanga njama hizo alifanikiwa kumchukuwa mtoto huyo Mei 15, 2024 na kwenda kumficha kwa rafiki yake aitwaye Hamida Gaudence Njuu anayeishi Jijini Mbeya.

Sambamba na hilo amesema Ufuatiliaji ulifanyika na Mei 24, 2024 majira ya saa saba kasoro usiku (00.45) mtoto huyo alikutwa nyumbani kwa Hamida Gaudence Njuu huko Simike Mbeya.

DCP Misime amesema tukio hilo limechukuwa muda mrefu kutokana na kila ambalo Polisi walikuwa wanapanga kwa kumshirikisha mama mzazi wa mtoto huyo wakidhani ana uchungu na mtoto wake lakini yeye akimfikishia taarifa mtuhumiwa mwenzake hivyo kumfanya aendelee kujificha.

Aidha amesema Jeshi hilo linawashikilia Watuhumiwa hao watatu kwa ajili ya kukamilisha taratibu zingine ili wafikishwe katika vyombo vya Sheria.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa watu wenye tabia kama hizi wafahamu watajificha kwa muda, iwe wiki, miezi au miaka ambapo alibainishakuwa Jeshi hilo litawakamata

Vile vile Msemaji wa Jeshi hilo alibainisha kuwa watu wafahamu fika vitendo kama hivi vya kula njama, kuteka, na kujiteka ni uhalifu ambao haulipi kwani mwisho wake kama Mungu ataendelea kukuweka hai lazima utakamatwa huku akisema mbaya zaidi inaweza kupelekea familia yako kusambaratika.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents