Habari

Mdogo wa RC Rukwa ajinyonga kukwepa deni la boda boda

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Litapunga, wilayani Mpanda mkoani Katavi, Agustino Wangabo (53) ambaye pia ni mdogo wake na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mhe. Joachim Wangabo, amejinyonga hadi kufa kwenye paa la nyumba yake kwa kutumia mkanda wa suruali kisa kikiwa ni kukwepa deni la pikipiki.

Tokeo la picha la sanlg motorcycle

Diwani wa kata ya Uwanja wa Ndege, Stephano Asalile, akielezea tukio hilo, amesema marehemu kabla ya kuchukua uamuzi wa kujinyonga, alikuwa akidaiwa na mtendaji mwenzake wa Kata ya Katumba, Tsh. milioni 1.6 tangu Agosti mwaka huu, baada ya kumuuzia pikipiki aina ya SAN-LG.

Bw. Asasile amesema baada ya mauziano hayo, Wangabo aliombwa na mteja wake ampatie kadi ya pikipiki, lakini hakumpa, hivyo akaomba apewe pikipiki hiyo kwa lengo la kwenda nyumbani kwake kuchukua kadi ili amkabidhi.

Kwa mujibu wa maelezo ya Asalile, amesema pamoja na Wangabo kuwa amelipwa fedha, hakukabidhi pikipiki hiyo toka Agosti na badala yake alitafuta mteja mwingine na kumuuzia pikipiki hiyo na hakurejesha fedha alizokuwa amechukua kwa mteja wake wa awali.

Kutokana na kitendo hicho, Mteja wake wa awali ambaye ni mtendaji mwenzake alianza kufanya jitihada za kudai arejeshewe fedha zake, lakini aliendelea kumpiga danadana na hakuonyesha dalili za kurudisha fedha hizo.

Bw. Asalile amesema hali hiyo ilimfanya achukue uamuzi wa kutoa taarifa polisi ndipo juzi mteja huyo alikwenda akiwa na polisi nyumbani kwa Wangabo kwa lengo la kufuatilia haki yake.

Asalile amesema wakati wakiwa karibu na kuifikia nyumba ya Wangabo, walimwona akiwa barabarani akila maandazi na alipowaona, alitimua mbio na kukimbilia ndani ya nyumba yake.

Polisi walitafuta uongozi wa serikali ya mtaa kwa lengo la kufanya upekuzi ili kumsaka ndani ya nyumba. Walipoingia ndani ya chumba chake, walimwona akiwa ananing’inia juu ya mtambaa wa paa la nyumba yake akiwa amejinyonga hadi kufa.” amesema Asalile.

Tayari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho ambacho alisema kimetokana na kujinyonga kwa kutumia mkanda wa suruali siku ya  Jumatatu majira ya saa 7:30 mchana katika mtaa wa Airtel, Kata ya Uwanja wa Ndege, Mpanda.

Wangabo ambaye ni mdogo wake na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Chanzo:Nipashe

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents