Habari

Mfahamu Brian Deacon, Muigizaji wa filamu ya Yesu aliyeishi maisha ya kipagani na baadae kuokoka

Muigizaji wa filamu, Brian Deacon ambaye ndiye aliyeigiza filamu ya Yesu (Jesus) alizaliwa mnamo tarehe 13/02/1949 huko Oxford nchini Uingereza akiwa ni mtoto wa pili katika familia yao, baba yake akiwa fundi makenika na mama yake akiwa ni Nesi.

Brian alipita kwenye mchujo mkali wa waigizaji zaidi ya 1000 ambao walifanyiwa mahojiano huku 260 wakijaribishwa kuigiza (screen test) kuona kwamba wanafaa, ambapo yeye akiwa ni mwingereza pekee kati ya waigizaji Waisrael walioingia kwenye usaili huo akiwa chini ya kampuni iitwayo New shakespears ambako alikuwa akifanya sanaa za majukwaani na uigizaji.

Akihojiwa na BBC, Brian amesema kabla ya kuchaguliwa mtihani wake wa kwanza ulikuwa kutoka kwa wakala wake aliyemvunja moyo kwa kumweleza kuwa kama ataweza kuigiza kama Yesu.

Hata hivyo, baadae alifanikiwa na baada ya hapo akawa na wakati mgumu kutoka kwa watu ambao kila mmoja alikuwa anajaribu kumweleza jinsi anavyotakiwa kuigiza sauti yake na mambo mengine, ingawa yeye alisema atatumia sauti yake na maelezo kutoka kwa muongozaji.

Brian amesema wiki tatu kabla hawajaanza kurekodi filamu hiyo, alisoma kitabu cha Luka mtakatifu zaidi ya mara 20 kwa kuwa filamu hiyo imenukuliwa kutoka katika kitabu hicho.

Kusoma kwake huko amedai kulimpa nguvu na moyo wa kuigiza filamu hiyo na kuweza kumfahamu vyema Yesu Kristo kuwa ni mtu wa aina gani.

Brian amesema walitumia miezi 7 kuigiza filamu hiyo, walikuwa wanaigiza kwa masaa mengi kuanzia saa kumi za alfajiri, alichokuwa anashangaa ni nguvu za ajabu alizokuwa akizipata na kuendelea kuigiza ingawa wakati huo anadai alikuwa mkristo jina wa kanisa katoliki.

Siku moja anasema wakati anaigiza alikuwa anawaombea watu mara mwanamke mmoja alishika mkono wake kumbe alikuwa na mapepo alimuombea na mapepo yalimtoka mwanamama huyo jambo ambalo lilimfanya aokoke baada ya kumaliza kuigiza filamu hiyo.

Siku nyingine waliokuwa wakiigiza kama wanafunzi wa Yesu wapatao 12 wakiwa ndani ya basi walikuwa wamepanga kugoma kutokana na malipo waliyokuwa wakipata, cha ajabu Director alikuja kumuomba (Brian) azungumze nao warejee kazini akashangaa akamwambia mimi sio Yesu ni Brian Deacon, akaamua kuzungumza nao na baada ya masaa 36 walikubali kurudi kuendelea na kazi.

Amesema mtihani mwingine ni siku alipokuwa hotelini mjini Tel Aviv, ambapo hoteli aliyofikia iliwaka moto, anasema bahati nzuri wote walitoka salama na kesho yake asubuhi waliendelea na kazi.

Brian amesema siku hiyo mmoja wa waigizaji anayeitwa, Tom Panella alianzisha mada kwa kusema moto uliokuwa umetokea ni hila za shetani na kusababisha mjadala wa muda mrefu ni vipi shetani anahusishwa kwenye swala hilo, lakini jibu likawa shetani hataki filamu hiyo irekodiwe ndio maana analeta hila zake.

Haikuwa kazi rahisi kurekodi filamu hiyo ukizingatia kipindi hicho teknolojia ilikuwa ni duni, baada ya kumaliza kurekodi kwa takribani miezi 18 filamu hiyo ilianza kuonyeshwa kwa baadhi ya watu na ndipo hata yeye kwa mara ya kwanza akaona ni kwa jinsi filamu hiyo ilivyokuwa na nguvu.

Baada ya filamu hiyo, Brian anasema alirudi kuigiza majukwaani na kwenye runinga, ambapo kwa miaka zaidi ya 30 sasa tangu kutoka filamu ya Yesu tayari imetazamwa na watu zaidi ya bilioni tatu duniani kote katika nchi 233 (kwa takwimu za mwaka 2001).

Filamu hiyo ambayo ilitengenezwa chini ya Campus Crusade for crusade ambao kwasasa wanaitwa Life Ministry pia nchini Tanzania wapo chini ya mkurugenzi Dismas Shekhalage, ambapo tayari imetafsiriwa katika lugha zaidi 500 huku nyingine zaidi ya 200 zikiwa njiani kutafsiriwa.

Brian anawaambia watu kwamba yeye ni mwigizaji tu na sio Yesu kama watu wengi wanavyomchukulia.

Anasema ameendelea kupata barua pepe mbalimbali za kumpongeza na kumshukuru kwa kazi nzuri aliyofanya kwenye filamu hiyo, ambapo kwa upande wake anasema anayo nakala ya filamu hiyo kwenye maktaba yake nyumbani kwao Uingereza kwa takribani miaka 20 .

Filamu nyingine alizowahi kushiriki ni pamoja na A zed & Two Noughts ya mwaka 1985, The Feathered Serpent ya mwaka 1976-1978 na Tamthilia ya iitwayo Lillie iliyoigizwa mwaka 1978 akitumia jina la Frank Miles.

Huyo ndiye Brian Deacon mwigizaji mkuu wa filamu ya ”JESUS” iliyoigizwa mwaka 1979 huko nchini Israel.

MAISHA YAKE KWA SASA:

Kwa sasa ni mzee ingawaje bado anajihusisha na masuala ya filamu na mwaka 2013 alicheza filamu ya mwisho ya Mistaken.

Alifunga ndoa yake ya kwanza na Rula Lenska ambapo alizaa naye Mtoto mmoja, Lara Deacon na ndoa yake ya pili alioana na mwanamama, Natalie Bloch mnamo mwaka 1998 .

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents