Habari

Mo Dewji akumbuka tukio la kutekwa kwake mwaka mmoja uliopita, Fahamu kesi ya kutekwa kwake ilipofikia

Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mo Dewji amekumbuka tukio la kutekwa kwake mwaka mmoja uliopita na kutoa shukrani kwa watu wote waliosaidia kupatikana kwake.

Mo Dewji kupitia kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Amesema kuwa tukio hilo lilikuwa ndio tukio baya zaidi kuwahi kutokea katika maisha yake.

Mwaka mmoja uliopita siku kama ya leo nilitekwa. Siku 9 nilizofungwa macho na mikono kilikuwa ni kitendo cha mateso zaidi kwenye maisha yangu yote. Kutokuwa na uhakika wa kuona dakika inayofata nikiwa hai ilikua ni hali ya kutisha, lakini nashukuru Mwenyezi Mungu, na sala za wengi, nilivuka shida zote. Kurudi kwangu salama ndio ushuhuda wa kweli wa nguvu ya maombi! Nilibarikiwa kwa kupewa nafasi ya pili ya maisha. Asanteni Watanzania wenzangu wote na kila mtu duniani kote kwa maombi yenu na msaada usio na shaka. Mwenyezi Mtukufu awasimamie katika mambo yenu kwa upendeleo mkubwa! Ameen,“ameandika Mo Dewji.

Mnamo tarehe 11, Oktoba mwaka 2018, katika maeneo ya Masaki Jijini Dar Es Salaam, Mfanyabiashara huyo alivamiwa na kutekwa na baadae siku 9 mbele aliachiwa huru.

JE, SAKATA HILO LIMEISHIA WAPI?

Mpaka sasa watu watu 6 wamekamatwa na upelelezi unaendelea, Ambapo mnamo Septemba 30 mwaka huu, Wakili wa Serikali, Daisy Makakala akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi ,alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na ameiomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Katika hatua nyingine wakili huyo alidai kuwa bado wanaendelea kuwatafuta washtakiwa wengine ili waunganishe katika kesi hiyo.

Awali mahakama hiyo ilitoa hati ya kuwakamata washitakiwa hao ambao ni Henrique Simbine, Daniel Manchice, Issac Tomo na Zacarious Junior wote raia wa Msumbiji na Phila Tshabalala raia wa Afrika Kusini.

Mmoja wa washtakiwa hao alifikishwa mahakamani hapo ni dereva wa taksi, mkazi wa Tegeta Mousa Twaleb. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Oktoba 15 mwaka huu.

 

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents