Habari

Rais Samia afunguka wanaodai ameuza bandari, apongeza TPA kutoa gawio la Bilioni 153.9

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa anaipongeza Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kutoa gawio kwa serikali kiasi cha Bilioni 153.9 na kwamba wanaopiga kelele kuwa ‘mama kauza bandari’ ni wazi kuwa wameona faida ya uwekezaji uliyofanywa bandarini hapo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati wa halfa ya kukabidhi gawio kwa serikali kutoka kwenye mashirika ya umma na binafsi, hafla hiyo yenye kauli mbiu ‘Mageuzi ya mashirika ya umma na wajibu wa kuchangia maendelwo ya Tanzania.

Amesema anaamini kuwa TPA itaendelea kupata faida na kutoa gawio kubwa zaidi kwa serikali hasa kutokana na mageuzi hayo yaliyofanyika.

“Pongezi maalum kwa makampuni yaliyoleta gawio kwa serikali ikiwemo TPA ambayo nina uhakika mwaka jana hii haikuwa level yenu, lakini kwa mageuzi yaliyotokea bandarini mmeweza kufikia kiwango hiki na mwakani nina uhakika mnaweza kuleta double ya mlichokitoa leo.

“Huko ndiko tulikuwa tunaelekea ndugu zangu, wale waliokuwa wanapiga kelele mama kauza bandari, mama kauza bandari, mama kauza nini, mauzo yale faida yake ni hii hapa na huu ni mwanzo tu tunatarajia kupata faida kubwa zaidi,” amesema Rais Samia

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu aliwataka watendaji wakuuu na Wakurugenzi wa mashirika ya umma wawe tayari kwa mabadiliko yatakayowawezesha kubadili namna yao ya kuendesha mambo na kutoa gawio kwa serikali.

Amesema watendaji hao kuhakikisha wanaongeza ubinifu na kukuza mapato ya taasisi zao ili yaweze kuingia kwenye mfuko mkuu wa serikali na kusaidia katika maendeleo ya Taifa

“Gawio linatolewa na taasisi za umma ni chini ya asilimia tatu na hivyo lazima mabadiliko makubwa yafanyike kufikia lengo la serikali la kupata gawio kwa asilimia 100,” amesema Mchechu.

Amesema taasisi ambazo serikali ina asilimia ndogo inachangia fedha nyingi katika mfuko mkuu wa serikali tofauti na mchango mdogo unatolewa na taasisi zinazomilikiwa na serikali kwa asilimia 100.

Ameongeza kuwa ofisi yake imekusudia kuja na mfumo thabiti ili kusaidia serikali kufanya uamuzi sahihi wakati wa uteuzi wa viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali.

Mchechu amesema mifumo hiyo itaondoa changamoto ya kuteua na kutengua ndani ya muda mfupi baada ya kuteuliwa.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents