Habari

Rais Samia: Nimejigeuza chura kiziwi sisikii wala siwajibu wanaonitukana

RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kazi ya mageuzi ya kiuchumi anayoifanya hapa nchini inasababisha anatukanwa na kupigiwa kelele nyingi lakini amejigeuza chura kiziwi ambaye atosikiliza mambo hayo bali ataendelea kutimiza malengo na mipango yake.

Rais Samia ameyasema hayo leo Ikulu, jijini Dar es Salaam wakati wa halfa ya kukabidhi gawio kwa serikali kutoka kwenye mashirika ya umma na binafsi, hafla hiyo yenye kauli mbiu ‘Mageuzi ya mashirika ya umma na wajibu wa kuchangia maendelwo ya Tanzania’.

Amesema anayasikia matusi anayotukanwa lakini amejigeuza chura kiziwi ambaye hayasikii wala kujibu bali anachotaka ni mageuzi ya kiuchumi ndani ya nchi ili maendeleo yapatikane.

“Kulikuwa na mashindano ya chura, waliwekewa tageti atakayefika juu atapatiwa zawadi, walipoanza kupanda huku chini watazamaji wakaanza kuwaambia shukeni ni hatari hamtaweza kufika mtashindwa tu, kelele zilikuwa nyingi kama zinazopingwa humu ndani kwetu, kwahiyo chura mmoja mmoja akaanza kushuka ila akabaki mmoja akaulizwa umewezaje kufika kumbe yule chura kiziwi asikii.

“Mimi kazi mliyonipa nasimama na naifanya na mnashuhudia matusi ninayotukanwa, mpuuzi huyo hana maana huyu bibi mambo chungu nzima lakini najigeuza chura kelele zinapigwa nyingi wakiona haujibu wanasema sasa tulitukane litajibu mimi sijibu masikio sisikii kabisa anayetaka kunikera anikanyagie uchumi wangu,” amesema Rais Samia

Rais Samia amesema kuwa kwenye mageuzi haya Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu na Waziri wake wanatakiwa kuendelea kufanyakazi kwakuwa anajua kuwa watachukiwa na kulaaniwa na baadhi ya watu wasiopenda kufanya kazi.

“Kwenye mageuzi haya Mchechu na Waziri wako lazima muwe ‘unpopular, sijawahi kusikia Waziri wa fedha akasifiwa hata siku moja siku zote analaaniwa, kwahiyo Mchechu najua hapa utalaumiwa, lawama zingine zitakuja personal nyingine kikazi lakini hii ndiyo kazi niliyokupa,” amesema na kuongeza

“Kwenye mageuzi haya tutakanyaga nguru wa mshihiri, kwahiyo anayetaka kunikera mimi anikanyagie uchumi wangu, najua katika mageuzi haya tutawakanyanga wengi hasa wale ambao hawataki kwenda mbele na ndio watapiga kelele nyingi sana, mliopo kwenye shirika ambao hamtaki kukanyagiwa nguru wenu nendeni mkafanye kazi ili kuleta maendeleo,” amesema Rais Samia

Kwa upande wake Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu aliwataka watendaji wakuuu na Wakurugenzi wa mashirika ya umma wawe tayari kwa mabadiliko yatakayowawezesha kubadili namna yao ya kuendesha mambo na kutoa gawio kwa serikali.

Amesema watendaji hao kuhakikisha wanaongeza ubinifu na kukuza mapato ya taasisi zao ili yaweze kuingia kwenye mfuko mkuu wa serikali na kusaidia katika maendeleo ya Taifa

“Gawio linatolewa na taasisi za umma ni chini ya asilimia tatu na hivyo lazima mabadiliko makubwa yafanyike kufikia lengo la serikali la kupata gawio kwa asilimia 100,” amesema Mchechu.

Amesema taasisi ambazo serikali ina asilimia ndogo inachangia fedha nyingi katika mfuko mkuu wa serikali tofauti na mchango mdogo unatolewa na taasisi zinazomilikiwa na serikali kwa asilimia 100.

Ameongeza kuwa ofisi yake imekusudia kuja na mfumo thabiti ili kusaidia serikali kufanya uamuzi sahihi wakati wa uteuzi wa viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali.

Mchechu ameema mifumo hiyo itaondoa changamoto ya kuteua na kutengua ndani ya muda mfupi baada ya kuteuliwa.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents