Habari

Serikali kuwezesha ujenzi wa shule za kata 226, nyumba za walimu 184

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema katika kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na ualimu, serikali itawezesha ujenzi wa shule za sekondari za kata 226, nyumba za walimu 184 wa sekondari pamoja na ununuzi wa vifaa vya maabara.

Hayo yamebainishwa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/2025.

Prof. Mkenda amesema serikali pia itawezesha ujenzi wa madarasa 2,018 (msingi 1,221 na sekondari 797), mabweni 114 kwa shule za sekondari; nyumba za walimu 658 (msingi 567 na sekondari 81) matundu ya vyoo 2,848 (msingi 1,514 na sekondari 884), maabara 10 na vituo vya walimu (TRCs) 300 kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Aidha, amesema itakamilisha ujenzi vyumba vya madarasa 111 katika shule za msingi 37, matundu ya vyoo, maabara, nyumba za walimu na mabweni katika shule za sekondari 50.

“Pia itaweka nishati safi ya kupikia ili kuendelea kuhifadhi na kuimarisha mazingira katika vyuo vya ualimu 11 (Nachingwea, Katoke, Kleruu, Tabora, Dakawa, Patandi, Mpwapwa, Sumbawanga, Mhonda, Kasulu na Monduli). Vilevile, itanunua samani kwa ajili ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga, Mhonda, Dakawa na Ngorongoro,” amesema Prof. Mkenda

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents