Habari

Serikali yaanza uchunguzi wa mifumo viwanja vya ndege

Serikali imeanza uchunguzi maalumu wa mapungufu mbalimbali katika Viwanja vyote vya ndege nchini ili kubaini changamoto na kuweza kuzifanyia kazi.

Imesema mapungufu ambayo yatafanyiwa kazi ni ya kimfumo, utendaji na upungufu wa miundombinu ili kuweza kuboresha sehemu husika lengo ikiwa kurahisisha uingiaji na utokaji wa wageni ikiwemo watalii wanoukuja nchini kwa shughuli za utalii ambao uiingizia nchi kiasi kikubwa cha fedha.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje,Ulinzi na Usalama ambapo kamati hiyo ilitembelea na Kukagua Mifumo ya Uhamiaji Mtandao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume,Ujenzi wa Chuo cha Uhamiaji Kitogani na Ujenzi wa Ofisi ya Uhamiaji mkoa wa Mjini Magharibi Mazizini.

Amesema uchunguzi huo unalengo pia kudhibiti uhalifu unaotokea katika viwanja vya ndege ikiwemo utoroshaji wa vito vya thamani, mnyororo wa upitishaji na uingiaji wa dawa za kulevya na uingiaji nchini kwa wageni bila kufuata sheria na taratibu za kiuhamiaji.

‘Mbali ya kazi nzuri ambazo zinafanywa na Uhamiaji lakini kuna maeneo tunataka kupeleka nguvu zaidi hasa maeneo ambayo kwanza ni sura ya nchi,malango makuu ya kuingilia kama hapa tulipo katika maeneo ya Viwanja vya Ndege,mtu akija Tanzania sura ya nchi inamuonyesha anapopokelewa katika viwanja vya ndege,haipendezi mgeni akija hapa nchini apange mstari mrefu,mara viyoyozi havifanyi kazi ndio maana serikali kuna uchunguzi maalumu tunafanya ili kuweza kubaini mapungufu hayo na kuyafanyia kazi katika Viwanja vyote vya ndege nchini.’ amesema Waziri Masauni

Akizungumza katika ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje,Ulinzi na Usalama,Vicent Mbogo amesema ni muhimu mapungufu hayo katika viwanja vya ndege yakafanyiwa kazi huku akisifu juhudi za serikali zote mbili katika kuiletea Zanzibar maendeleo ambapo alisema Zanzibar ni nchi ya utalii ni vyema huduma malango ya nchi zikaboreshwa.

‘Zanzibar imeendelea kwa kasi kubwa pamoja na maendeleo haya ya miundombinu katika uwanja wa ndege ambapo sasa yanasomana na kule Tanzania Bara tumeona maendeleo yanafanyika katika viwanja vyetu ambavyo ndio maingilio ya watalii ambao wanatuletea fedha nyingi hapa nchini,napenda kwapongeza Marais wetu,Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt.Hussein Ali Mwinyi wanafanya kazi kubwa sana kuiletea nchi yetu maendeleo’alisema Mbogo

Naye Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar,Hassan Ali Hassan alitaja jinsi miradi ya maendeleo ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 ilivyokamilika ikiwemo Ujenzi wa Ofisi ya Uhmiaji mkoa wa Mjini Magharibi,Mkoa wa Kusini Pemba,Ukarabati wa Ofisi Kuu ya Uhamiaji Zanzibar,Ukarabati wa Nyumba ya Makazi ya Askari Ndugu Kitu Chake Chake Pemba na Ukarabati wa Nyumba Mbili za Makaazi ya Askari Mtemani Wete na Pemba ambapo imekamilika kwa asilimia mia moja huku gharama yake ikiwa ni kiasi cha Shilingi Bilioni1.9.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents