Siri yafichuka mfumo wa oksijeni kwenye ndege aina ya Boeing 787 watiliwa shaka, Fahamu zaidi – Video

Siri yafichuka mfumo wa oksijeni kwenye ndege aina ya Boeing 787 watiliwa shaka, Fahamu zaidi - Video

Mfichua siri wa Boeing amedai kuwa abiria katika ndege ya 787 Dreamliner huenda wakaachwa bila hewa ya oksijeni ndege hiyo ikipata ghafla hitilafu ya kiufundi. John Barnett anasema uchunguzi umebaini kuwa hadi robo ya mfumo wa oksijeni una hitilafu na kwamba huenda ikakosa kufanya itakapohitajika.

Pia anadai kuwa vipuri vya ndege vilivyo na kasoro vimewekwa wakati ndege hiyo ilipokuwa ikiundwa katika kiwanda cha Boeing.

Boeing imepinga madai hayo ikisema kuwa ndege zake zote zinaundwa kwa kuzingatia viwango vy usalama vya hali ya juu.

Kampuni hiyo imejikuta mashakani siku za hivi karibuni baada ya ajali mbili mbaya zilizohusisha ndege yake ya 737 Max -iliyokuwa ya shirika la ndege la Ethiopia na kupata ajali mwezi Machi na ajali ya Lion Air ya Indonesia mwaka jana.

Bwana Barnett, ni injinia wa zamani wa udhibiti wa ubora, aliyefanya kazi na Boeing kwa miaka 32, hadi alipostaafu kwa misingi ya afya yake mwezi March mwaka 2017.

Kutoka mwaka 2010 aliajiriwa kama meneja anayesimamamia masuala ya ubora wa viwango vya uundaji ndege katika kiwanda cha Boeing cha North Charleston,Kusini mwa jimbo la Carolina.

John BarnettJohn Barnett injinia wa zamani wa udhibiti wa ubora, katika shirika la Boeing

Kiwanda hicho ni moja ya viwanda vilivyohusika na uundaji wa 787 Dreamliner, inayotajwa kuwa ndege ya kisasa ya aina yake ambayo hutumika sana kwa safari ndefu kote duniani

Licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa baada ya kuanza huduma zake ndege hiyo ilivutia mashirika kadhaa ya ndege kuimiliki, na imekuwa chanzo cha faidi kwa mashirika hayo.

Lakini kwa mujibu wa Bw. Barnett, 57, kinyang’anyiro cha ununuzi wa ndege hiyo mpya ilisababisha uundaji wake kuharakishwa, hali ambayo huenda ilifanya viwango vya usalama wake kutozingatiwa kikamilifu.

Shirika la Boing limepinga kauli hiyo na kusisitiza kuwa “usalama, ubora na uadilifu ni msingi wa utendakazi wa Boing”.

 

Mwaka 2016, anaiambia BBC, kuwa aligindua tatizo la kiufundi katika mfumo wa oksijeni ambayo inastahili kuwasaidia abiria na marubani kupata hewa endapo ndege itakumbwa na hitilafu ikiwa angani kutokana na sababu yoyote.

Mirija ya kupumulia hewa safi inatarajiwa kuning’inia kutoka juu ya ndege, ambayo inasaidia kupata hewa ya oksigeni.

Bila mfumo kama huo, abiria watashindwa kupumua. Ndege ikiwa inapaa umbali wa futi 35,000, kutoka ardhini au juu ya bahari abiria watazirai kwa chini ya dakika moja.

Ndege ikiwa inapaa umbali wa futi 40,000, hali hiyo inaweza kujitokeza katika kipindi cha sekunde 20. Wakati huo ubongo utaathiriwa na huenda abiria wakafariki.

Ndege ya aina ya Boeing 737-700 ya shirika la ndege la Southwest ikiwa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Philadelphia baada ya kulazimika kutua ilipokumbwa na hitilafu katika injini yake April 17, 2018.Ndege ya aina ya Boeing 737-700 ya shirika la ndege la Southwest ikiwa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Philadelphia baada ya kulazimika kutua ilipokumbwa na hitilafu katika injini yake April 17, 2018.

Bwana Barnett anasema wakati alipokuwa anarekebisha mfumo wa hewa ndani ya ndege ulioharibika aligundua kuwa baadhi ya mitungi ya kusambaza hewa ya oksijeni ilikuwa haifanyi kazi kama inavyostahili.

Alipokuwa akifanyia marekebisho mfumo huo aliifanyia majaribio kwa kutumia utafiti wa Boeing yenyewe ili kuiunda upya.

Uchunguzi huo ulifanywa kwa kutumia vifaa ambavyo “havitumiki” na vilivyoharibika, ulitengenezwa ili kuiga jinsi zitakavyotumika ndani ya ndege ikiwa safarini, kwa kutumia umeme kama kichocheo.

Anasema mifumo 300 ilifanyiwa majaribio na 75 kati ya hizo hazikufanya kazi vyema, kwa asilimia 25%.

Bwana Barnett anasema juhudi yake ya kushughulikia hitilafu hiyo ilipingwa na mameneja wa Boeing.

Ndege ya Boeing aina ya Dreamliner ikifanya safari yake ya kwanza mwaka 2009 na kutoka wakati huo ndege zaidi ya 800 zimenunuliwa na mashirika ya ndege tofauri dunianiNdege ya Boeing aina ya Dreamliner ikifanya safari yake ya kwanza mwaka 2009 na kutoka wakati huo ndege zaidi ya 800 zimenunuliwa na mashirika ya ndege tofauri duniani

Mwaka 2017,aliwasilisha suala hilo kwa Utawala wa safari za anga nchini Marekani-Federal Aviation Administration (FAA), kwamba hakuna hatua iliyochukuliwa kurekebisha hitilafu hiyo.

Lakini FAA, hatahivyo ilisema kuwa haiwezi kuthibitisha madai hayo, kwasababu Boeing ilisema itashughulikia suala hilo wakati huo.

Boeing yenyewe imepinga kauli ya Bw. Barnett.

Ilikubali kuwa mwaka 2017 “iligundua kuwa baadhi ya mikebe ya oksijeni waliyopokea kutoka kwa wasambazaji wao zilikuwa hazifanyi kazi vizuri. Tuliondoa chupa hizo katika kiwanda chetu cha kuunda ndege na hata zile zikuwa zimetumiwa wakati wa uundaji wa ndege zilizotanzgulia na kuwasilisha malalamiko yetu kwa wasmbazaji hao”.

Lakini pia ilisema kuwa “mfumo wa hewa ya oksijeni ya kila abiria iliyowekwa katika ndege yetu imefanyiwa uchunguzi mara kadhaa kabla ziwasilishwe ili kuhakikisha zinafanya kazi vyema, na lazima zipite uchunguzi huo kabla kuwekwa kwenye ndege.”

“Mufumo huo pia unafanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara hata baada ya ndege kuanza kuhudumu,” ilisema.

Jengo la Utawala wa safari za anga nchini Marekani-Federal Aviation Administration (FAA)Jengo la Utawala wa safari za anga nchini Marekani-Federal Aviation Administration (FAA)

Haya sio madai pekee yaliyoelekezwa kwa Boeing kuhusu kiwanda chake cha kuunda ndege cha South Carolina, hatahivyo. Bw. Barnet pia anasema kuwa Boeing ilikosa kuzingatia mwongozo wake binafsi, ambao unalenga kufatilia ubora wa vipuri vya ndege zake wakati zikiundwa, hali ambayo inaruhusu vipuri vilivyo na kasoro “kupita”.

Anadai kuwa wafanyakazi walio katika presha ya kufikia malengo ya kampuni wanaishia kutumia vipuri vya viwango vya chini kutoka katika jaa la taka ambalo liko karibu na eneo la kuundia ndege mpya.

Katika kisa kimoja hata afisa wa ngazi ya juu alijua kitu kama hicho kinafanyika. Anasema hatua hiyo ilichukuliwa ili kuokoa muda, kwa sababu “kiwanda cha Boeing cha South Carolina kinaeneshwa kwa ratiba na gharama ya uundaji wa ndege mpya”

Kuhusu suala la vipuri kupotea, mapema mwaka 2017 uchunguzi uliofanywa na Utawala wa safari za anga nchini Marekani ulithibitisha hofu ya Bw. Barnett.

Tangu wakati huo, kampuni hiyo inasema kuwa, “ilitatua kikamilifu matokeo ya FAA kuhusu ufuataji wa vipuri na kutekeleza mapendekezo yote ya ukarabati wa ndege ili kuzuia hitilafu kutokea tena”.

Haikutoa mailezo zaidi kuhusu uwezekano wa vipuri vilivyo na kasoro kutumiwa kuunda ndege mpya- japo vyanzo kutoka ndani ya kiwanda hicho cha North Charleston vinasema huenda hilo linafanyika.

The first South Carolina-built Boeing 787Kiwanda cha Boeing cha North Charleston mjini South Carolina ni moja ya viwanda vilivyounda 787 Dreamliner

Bw Barnett kwa sasa amechukua hatua za kisheria dhidi ya Boeing, ambayo analaumu kwa kumharibia sifa na kusambaratisha taaluma yake kutokana na masuala aliyofichua, na hatimae kushurutisha kustaafu mapema.

Kampuni ilijibu hoja hiyo kwa kusema kuwa injinia huyo alikuwa na mpango wa kustaafu kwa muda mrefu na kwamba alifanya hivyo kwa hiari.

Inasema kuwa “Boeing haijaathiri kwa vyovyote uwezo wa bwana Barnett kuendelea na kazi yoyote aliyotaka kufanya hata baada ya kuondoka katika kampuni hiyo”.

Chanzo BBC.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW