Habari

Tanzania na Saudi Arabia kushirikiana katika sekta ya mafuta na gesi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali ina nia ya kuimarisha miundombinu ya maghala ya kuhifadhia mafuta kwenye bandari za Tanga na Mtwara.

Amesema hayo leo Juni 19, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na Mbunge wa Bunge la Maldives, Mhe. Ibrahim Muhammad.

“Kwa miaka miwili sasa Tanzania inashirikiana na Saudi Arabia kupitia Kampuni yake ya ARAMCO, huu ni ushahidi wa uhusiano wetu imara. Kwa sasa maghala yetu makubwa yapo Dar es Salaam hata hivyo tuna nia ya kupanua miundombinu ya maghala yetu ya kuhifadhi mafuta katika bandari ya Tanga na Mtwara. Upanuzi huu utaimarisha uwezo wetu wa usambazaji wa mafuta nchini,”amesema Dkt. Biteko.

Aidha, kuhusu gesi Dkt. Biteko ametaja baadhi ya fursa hasa katika gesi iliyoshindiliwa (CNG) na kuwa Serikali imeendelea kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Tanzania imeanza Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia ikilenga kuondoka kwenye matumizi ya nishati zisizo salama kwa mazingira kama vile kuni na mkaa, kadhalika tunachochea matumizi ya gesi asilia kwenye magari kama mbadala wa mafuta. Tunafahamu kuwa kwa sasa ni asilimia 6 tu ya wananchi ndiyo wanatumia gesi kupikia, Serikali ina mpango wa kuchochea matumizi haya na kufikia asilimia 80 kufika mwaka 2034, ili kufikia lengo hili serikali ya Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na wadau mbali mbali ikiwemo Saudi Arabia pamoja na Maldives ili kufikia malengo tuliyojiwekea ndani ya muda mfupi.” Amesema Dkt. Biteko.

Akizungumzia uwekezaji katika kiwanda cha kuzalisha dawa za kuku, Dkt. Biteko amewakaribisha wawekezaji wa dawa hizo kutoka nchini Misri na kusema kuwa Tanzania na Misri ni washirika wa muda mrefu na nchi hizo zina uhusiano wa kihistoria na kuwa Tanzania ni nchi nzuri ya kuwekeza kwa kuwa ina soko la uhakika na mazingira wezeshi ya kuwekeza.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Bunge la Maldives, Mhe. Ibrahim Muhammad ameeleza nia yake ya kuwekeza katika sekta ya nishati nchini Tanzania kupitia nchi ya Saudi Arabia na kusema kuwa uwekezaji huo utaimarisha uhusiano wa nchi hizo tatu.

Aidha, kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Musa Zungu na ujumbe kutoka nchini Misri.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents