Habari

Mashindano ya Netiboli Africa yaanza Tanzana Leo


PAZIA la michuano ya Netiboli Afrika, linafunguliwa leo kwa michezo miwili, ambapo wenyeji Tanzania (Taifa Queens) waitaivaa Lesotho, huku mabingwa watetezi, Malawi wakiikabili Botswana kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Mke wa Rais, Salma Kikwete ndiye atakayekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mashindano hayo yaliyopata mwitikio wa nchi saba, ambazo mbali na Tanzania zingine ni Malawi, Botswana, Lesotho, Zimbabwe, Zambia na Uganda.

Kocha wa Taifa Queens, Mery Protas amesema hana wasiwasi na maandalizi ya kikosi chake kwenye michuano hiyo, na amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia.

Protas alisema anategemea wachezaji watafuata maelekezo yake na kufanya vizuri kwenye mashindano hayo yanayotarajia kuwa na ushindani mkubwa.

“Tulikuwa na tatizo la pumzi, lakini mechi tatu za kirafiki tulizocheza na timu ya wanaume ya Zanzibar (JKU) zimesaidia kupunguza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa,” alisema Protas.

Endapo Queens itashinda medali mojawapo kati ya tatu, itakata tiketi ya kushiriki kwa mara ya kwanza michezo ijayo ya Jumuiya ya Madola.

Akizungumza jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Rose Mkisi alisema maandalizi yote kwa ajili ya mashindano hayo yamekamilika.

Mkisi aliwashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza kwa hali na mali kusaidia kufanikisha mashindano hayo, ambapo Sh158 milioni zilihitajika.

Katika hatua nyingine, Kampuni ya huduma za Simu za mkononi, Vodacom jana ilikabidhi vifaa vya michezo, jezi, viatu, tracksuit huku Zantel wakitoa simu 300 kwa wachezaji wote watakaoshiriki michuano hiyo mwaka huu.

Naye Mwenyeki wa Kamati ya Mashindano, mke wa Waziri mkuu Tunu Pinda amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kuishangilia timu ya taifa.

“Hakutakuwa na kiingilio hivyo ni vizuri wadau na mashabiki wa mchezo huu mkajitokeza kwa wingi na kuishangilia timu yetu ifanye vizuri na kutwaa kombe,” alisema.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents