Afisa mtendaji mkuu wa NMB atoa msaada Kilakala

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amefichua siri ya mafanikio yaliyopelekea kuongoza taasisi kubwa ya kifedha hapa nchini huku akiwataka wanafunzi kufuata nyayo zake hasa kwa kuzingatia masomo yao kwa kusoma kwa bidii na kuwa na nidhamu.

Bi.Ruth aliyasema hayo wakati akizungumza katika mahafali ya kidato cha nne Shule ya Sekondari ya wasichana wenye vipaji ya Kilakala mkoani Morogoro alipohudhuria shughuli hiyo kama mgeni rasmi.

Hata hivyo, Bi. Ruth ambaye ni mmoja kati ya wanafunzi waliosoma shuleni hapo miaka 30 iliyopita,  kwa niaba ya Benki ya NMB kupitia sera yake ya uwajibikaji kwa jamii, alitoa msaada wa meza 50, viti 50 vyenye thamani ya sh. Milioni 5 pamoja na kompyuta 10 ambazo kwa uhakika zitakuwa chachu ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na pia mazingira ya ufundishaji katika shule hiyo.

Nae Mkuu wa Shule – Bi. Mildreda Selula alimshukuru Bi. Zaipuna kwa niaba ya Benki yake kwa msaada huo kwani kwa kiasi kikubwa utapunguza uhaba waliokuwa nao, alisema kuwa shule ya Sekondari Kilakala itaendelea kufanya vizuri katika mitihani ili kuwatia  moyo wote wenye nia ya kuendelea kusaidia wakiwemo NMB.

Shule ya Kilakala ina jumla ya wanafunzi 657 huku wanafunzi wanaohitimu ni 88. Ina michepuo ya sayansi, biashara na sanaa kwa kidato cha kwanza hadi nne na kidato cha tano na sita kukiwa na tahasusi tatu za sayansi ambazo ni PCM, PCB na CNG na tahasusi moja ya sanaa ambayo ni HGL.

Related Articles

Back to top button