Burudani

BASATA yawapiga msasa viongozi wa vyama vya wasanii

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewapa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo katika maeneo mbalimbali viongozi wa vyama na taasisi zinazojihusisha na wasanii ili kujenga ufanisi zaidi katika sekta ya Sanaa.

DSC_0122
Katibu Mkuu wa BASATA, Godfrey Mngereza

Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Jumanne hadi Alhamisi ya wiki hii yalijikita katika kuwajengea uwezo Wasanii kwenye maeneo ya uandaaji bajeti, uandaaji wa mipango mikakati na sheria ya hakimiliki na hakishiriki na mikataba kwenye kazi za Sanaa.

Akizungumza kwenye hafla ya kuyafunga mafunzo hayo, Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza alisema kwamba ana matumaini makubwa kwamba mafunzo haya kwa viongozi wa wasanii yataamsha ari katika utawala na utendaji wa sekta ya Sanaa na kufanikisha kupiga hatua kwa sekta hii muhimu.

“Nina imani katika mafunzo haya tutawaona viongozi wa wasanii mnakuwa na mipango ya muda mrefu, wa kati na mfupi maana hakuna jinsi tunaweza kuwaongoza wasanii bila kuwa na mipango” alisisitiza Mngereza.

Kuhusu suala la hakimiliki, hakishiriki na mikataba kwenye kazi za Sanaa alisema kuwa ni tatizo linalowakumba wasanii wengi hivyo imani ya BASATA ni kuona viongozi hawa waliopatiwa mafunzo wanakuwa msaada kwa wasanii walio chini ya vyama vyao.

“Suala la hakimiliki linamgusa kila msanii, naamini kwenye suala hili mmejifunza vya kutosha. Aidha, mmejifunza suala la mikataba katika kazi za Sanaa, nawaomba muwe mabalozi katika kuwaelimisha wasanii umuhimu wa mikataba katika kazi wanazozifanya,” aliongeza Mngereza.

Awali akiongea kabla ya kukabidhi vyeti kwa washiriki, mgeni rasmi ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Shani Kitoga aliwataka viongozi hao kuzingatia mafunzo waliyoyapata na kuhakikisha wanakuwa mabalozi wa mabadiliko kwenye sekta ya Sanaa.

“Sanaa tunasema ni kazi hivyo lazima mafunzo haya mliyoyapata myatafsiri katika vitendo kwa kuonesha utendaji kazi ulio bora na unaozingatia mipango” alisema Bi. Kitoga.

Akiongea kwa niaba ya viongozi wa wasanii zaidi ya arobaini (40) waliohudhuria mafunzo hayo, Msanii mkongwe wa Sanaa za Maonesho Kassim Mbelemba maarufu kwa jina la Mzee Jangala alilipongeza BASATA kwa kuandaa mafunzo hayo na kuwaeleza wasanii kuwa sasa hakuna sababu ya kulalamika bali kuyafanyia kazi yale waliyojifunza.

Mafunzo haya ambayo ni sehemu ya kutekeleza mpango mkakati wa BASATA yaliwezeshwa na wakufunzi Rashid Masimbi ambaye ni mtaalam wa kuandaa mipango mikakati, Mrisho Mtumwa ambaye ni mtaalam wa kuandaa bajeti na John Kitime ambaye ni Msanii na mtaalam wa masuala ya hakimiliki na hakishiriki.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents