Habari

CCM: Tanzania haina tatizo la njaa

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa kwa sasa Tanzania haina tatizo la njaa, isipokuwa kuna upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo na endapo kungekuwa na baa hilo la njaa, mwenye mamlaka ya kulitangaza tatizo hilo ni mkuu wa nchi pekee.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam Jumatano hii na Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM), Humphrey Polepole alipozungumza kuhusu mwenendo wa hali ya siasa nchini.

“Ndio maana nasema CCM inatekeleza mfumo wa siasa safi na uongozi bora na mara zote hatupendi malumbano yasiyo na tija. Wapo baadhi ya wanasiasa na viongozi wa upande wa pili, wanaotumia fursa hii ya upungufu wa chakula kwa kueneza uzushi na uongo kwa wananchi kuwa kuna baa la njaa,” alisema.

Aidha Polepole alisema chama hicho kimebaini kuwa wapo viongozi ambao hawana hata taarifa za kutosha kuhusu suala hilo la chakula, lakini wanatumia fursa hiyo kueneza propaganda zao za kisiasa kwa maslahi yao.

“Naomba niwakumbushe kutoa taarifa za uongo zitakazoamsha taharuki miongoni mwa wananchi ni kosa la jinai. Zipo mamlaka zinazoweza kutoa vyema ufafanuzi kuhusu jambo hili. Nashukuru tayari serikali imeanza kufafanua na kubainisha hatua zinazochukuliwa kukabili hali hii,” alisisitiza.

“Yupo mwingine ametokea naye na kudai kuwa eti atawaombea chakula Watanzania na kuwagawia bure. Hivi taifa litaendeleaje endapo litakuwa na wananchi wasiofanya kazi wanaosubiri chakula bure? Naombeni Watanzania viongozi wa aina hii tuwapuuze”.

Siku chache zilizopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepinga kauli ya kusema Tanzania kuna balaa la njaa.

BY: Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents