Kenya: Mwalimu aeleza alivyoamua kufanya kazi za ndani ili kujikimu na maisha baada ya Corona kutokea

Macrine Otieno, aliyekuwa Mwalimu katika shule ya msingi ya kibinafsi ya Chrives Royal jijini Nairobi, lakini sasa kutokana na virusi vya Corona amelazimika kufanya kazi ya ujakazi ili ili kujikimu kimaisha.

Macrine ni mmoja wa maelfu ya walimu ambao wameathirika hata zaidi kutokana na kufungwa Kwa shule ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona mwezi wa Machi mwaka huu.

“Wakati shule zilipofungwa, mshahara ulisimamishwa kwa kuwa nilikuwa Mwalimu kwenye shule ya binafsi.”

Wanasema kwamba akiba haiozi, lakini akiba alizowekeza Macrine zilimsaidia kwa muda mchache kabla ya mtoto wake kuugua na kumlazimisha kutumia akiba hiyo kumtibu.

“Mtoto wangu aliugua kwa muda wa wiki tatu na kadi yangu ya bima ya matibabu nikawa nimeipoteza. Fedha zote nilizokuwa nazo kwenye akiba, nililazimika kuzitumia kumtibu mwanangu. Fedha zilizosalia nikatumia kulipia Kodi ya nyumba.”

Macrine Otieno

Hata hivyo, siku zilivyozidi mbele ndivyo maisha yalivyoendelea kuwa magumu kwake Macrine na mtoto wake. Chakula ikawa vigumu kupata pamoja na kodi ya nyumba.

“Nilianza kupokea ujumbe kutoka Kwa mwa nyumba, kwamba anataka Kodi. Huku chakula hata sikuwa nacho, hata cha kumlisha mtoto pekee. Baada ya siku chache , nikafungiwa nyumba…Nikawaza nitafute kazi ambayo itaniwezesha hata kupata fedha kidogo ambazo zingetuwezesha kuishi”

Mwalimu huyu ambaye amekuwa akifundisha kwa muda wa miaka 6 aliamua kutafuta kazi kama kijakazi kwa msingi kwamba kazi hiyo ingempa malazi na hata chakula.

Akamwomba rafiki yake amsaidie kumlea mtoto wake ili aweze kutafuta kazi hiyo ya ujakazi.

” Nilimchukua mtoto wangu nikampeleka Kwa rafiki yangu… Nilihisi kusikitika sana kwa sijawahi ilimaanisha kutengana na mwanangu tangu alipozaliwa. Lakini sikuwa na budi kwasababu nilifikiria maisha ya mtoto wangu, jinsi Kwa siku kadhaa tulikosa hata chakula. Na nikaamua kwamba nitafanya kazi yotote ilimradi nipate mapato yatakayoniwezesha kuanzisha biashara.” Alisimulia Macrine huku akilia.

Ninachokosa ni uhuru

Mwalimu Macrine Otieno alilazimika kumpa mtoto wake rafiki yake amsaidie kulea baada ya kukosa kazi
Mwalimu Macrine Otieno alilazimika kumpa mtoto wake rafiki yake amsaidie kulea baada ya kukosa kazi

Macrine aliweza kupata ajira. Baada ya siku chache akiwa kwenye kazi yake mpya, alipokea simu kutoka Kwa rafiki yake kwamba aende akamchukue mwanawe. Hili lilimfanya kuvunjika moyo hata zaidi Kwa kuwa, kazini, mwajiri wake hangemruhusu yeye kuishi na mwanawe.

Hivyo akalazimika kumpeleka kwa binamu yake. Hata hivyo haikuchukua muda, rais Uhuru Kenyatta akafungua mipaka ya kaunti iliyofungwa kwa ajili ya kudhibiti maaambukizi ya ugonjwa wa Corona. Macrine akamtuma binamu yake kumpeleka mtoto kwa wazazi wake Kwa sababu hangeweza kupewa ruhusa tena kazini.

“Ninachokikosa sana kwenye kazi hii ni uhuru… Ilikuwa ni vigumu sana Mimi kupata ruhusa ya kuenda kumchukua mwanangu, rafiki yangu aliponiita. Na wakati mipaka ilifunguliwa, nilinyimwa ruhusa ya kumpeleka mwanangu Kwa wazazi wangu. Kila unapotaka kufanya chochote, lazima uombe ruhusa, na ukinyimwa basi ndiyo hivyo… Huwezi kufanya lolote”

Kila Macrine alipoziba ufa mmoja, ili asijenge ukuta mwimgine ulijitokeza. Mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi Macrine, alivitupa nje vifaa vyake vya nyumba kwa kuwa alishindwa kulipa kodi ya nyumba. Na kwa kuwa ilikuwa vigumu kwake kupata ruhusa kazini, ilimbidi kuwapatia jirani zake vifaa hivyo.

“Nilipigiwa simu na jirani yangu akaniambia kwamba mwenye nyumba amevitoa vitu vyangu nje ya nyumba na nyumba imepewa mpangaji mwingine. Nilimwaambia anisaidie kuniwekea kile ambacho angeweza kukiweka, na vingine wagawane na jirani wengine wavitumie”

Ninachokikosa sana ni Uhuru…Ni maneno anayoisema Macrine Otieno, aliyekuwa Mwalimu katika shule ya msingi ya kibinafsi ya Chrives Royal jijini Nairobi. Ila sasa kutokana na virusi vya Corona amelazimika kufanya kazi ya ujakazi ili kujikimu kimaisha.

Katika maisha inabidi ujipange

Susan Manyala anayesimamia usajili katika kampuni ya kuwasajili vijakazi ya Nyarai Home of Humility, ambayo pia ni kampuni iliyomsajili Macrine anasema kwamba walipokea walimu wanne mwezi wa sita.

” Tumewasajili walimu 4. Tatu kati yao wameshapata ajira ila mmoja aliyesalia, imekuwa ni vigumu kwake kuajiriwa kwa madai kuwa ana umri mkubwa. Ana umri wa miaka 45, na wateja wengi wanashuku iwapo ataweza kufanya kazi za nyumba.”

“Wateja wanawafurahia sana kwasababu wanasema kwamba licha ya wao kufanya kazi za nyumba wanaweza pia kuwafundisha watoto wao”

Marima Otieno sasa anajiandaa kuanzisha biashara yake na fedha alizopata.
Marima Otieno sasa anajiandaa kuanzisha biashara yake na fedha alizopata.

Kazi ya ujakazi haijakuwa rahisi kwake Macrine, na ni matumaini yake kwamba mambo yatakuwa sawa, na hali itarejea kama ilivyokuwa awali.

“Inaniuma sana ila sina budi. Licha ya uchungu niaohisi, najua ni lazima nivumilie. Na nijajua ya kwamba nikitoka hapa tutakuwa pamoja na mtoto wangu. Ila nahisi kwamba siwezi kuendelea. Nasubiri fedha nitakazopata mwisho wa mwezi huu, ingawa kidogo nitaenda nianzishe biashara…”

“Katika maisha unapaswa ,uwe tayari ujipange, na ujue maisha hubadilika, leo inaweza kuwa sawa kesho ikawa hali tofauti, lakini kwa chochote kile ambacho kitatokea, ni vizuri tukubali na tutafute mbinu ya kujisaidia.”

Mapema mwezi huu, Wizara ya Elimu ncini Kenya ilitangaza kwamba shule zote za msingi na za upili (sekondari)zitafunguliwa Januari mwaka wa 2021, hatua ambayo walielezea wamechukua ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, hasa kwa watoto.

Siku mbili baada ya kufanya mahojiano haya na Macrine, alitupatia ujumbe kwamba ameiacha kazi hiyo na sasa anajiandaa kuanzisha biashara yake na fedha alizopata.

Related Articles

Back to top button