Habari

Lowassa awaandikia waraka waliotimuliwa CCM, awakaribisha Chadema

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) amewakaribisha waliokuwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba kujiunga na Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Lowassa amewaandikia waraka huku akisema kuwa walikuwa ni mashujaa waliosimama kupigania demokrasia ya kweli.
Alisema wanachama hao walikuwa mashujaa wa kutetea haki, demokrasia na taratibu kwa kupinga dhuluma ndani ya chama chao cha CCM.

“Nafsi yangu imenisukuma kushika kalamu na kuandika haya kutokana na kile kilichotokea Dodoma katika vikao vya CCM. Ni takriban miezi 20 sasa toka nilipojitoa CCM, lakini nasikia bado naendelea kutajwatajwa huko katika vikao vyao.”

“Wamewatimua wanachama na viongozi wao ambao wengi wao walitumia demokasia yao kupinga upindishwaji wa kanuni na sheria za chama chao.Nataka kuwaambia kuwa wakati wakifanya hivyo walikuwa mashujaa wa haki na demokrasia na misingi ya utawala bora nchini,” alisema Lowassa katika taarifa yake.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu alisema wanachama hao wa CCM walisimamia kile walichokiamini bila ya kuvunja sheria, wamekata minyororo ya unyonge na uonevu. Mbegu ile waliyoipanda itamea na kuzaa matunda demokrasia ya kweli nchini kwetu.

“Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba upinzani wa kweli utatokea CCM, naamini usemi huo sasa unatimia kwa kasi kubwa. Nawakaribisha Chadema na Ukawa kwa jumla huku kuna maisha mazuri sana, hakuna minyororo ya utumwa wa siasa. Kilichowapata ni sawa na kumpiga chura teke unamuongezea kasi tu.

“Waje wajiunge nasi katika safari ya kuleta demokrasia ya kweli na siasa zenye ukomavu, safari hii inahitaji umoja na mshikamano kufikia malengo. Nashangazwa na namna hatua ya CCM kujinasibu kuwa CCM ikiyumba.

Alisema nchi itayumba lakini anaamini kinachotokea na jinsi CCM inavyoyumba ndivyo wananchi wanavyozidi kukomaa katika siasa na kuimarika katika harakati za kutafuta mabadiliko ya kweli. Watanzania wa sasa hawawezi tena kuvumilia ukandamizaji wa haki zao za msingi unaofanywa na watawala.

“Nidhamu ya woga haina tena nafasi katika kujenga nchi yenye kuheshimu misingi ya haki demokasia na utawala bora,” alisema.

Juzi, CCM kilitangaza kuwafukuza wanachama wake 12, akiwamo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT), Sophia Simba, ambaye wiki iliyopita alitangaza kutogombea tena nafasi hiyo.

Wengine waliofukuzwa ni wenyeviti mikoa ambao ni Jesca Msambatavangu (Iringa), Erasto Kwilasa (Shinyanga), Ramadhan Madabiba (Dar es Salaam) na Christopher Sanya (Mara). Wengine ni Willfred ole Mollel ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini, mjumbe wa NEC wa Wilaya ya Babati Mjini, Ally Sumaye na Mathias Manga wa Wilaya ya Arumeru.

Katika orodha hiyo pia wamo wenyeviti wa wilaya wa chama hicho ambao ni Omari Awadhi (Gairo), Ally Msuya (Babati Mjini), Makolo Laizer (Longido) na Salumu Madenge (Kinondoni-Dar es Salaam).

Wanachama wengine waliochukuliwa hatua baada ya kufanya makosa kama hayo kuwa ni Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye amepewa onyo kali na anatakiwa kuomba radhi. Wakati Nchimbi akipewa onyo, Adam Kimbisa ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma na Mbunge wa Afrika Mashariki amesamehewa.

Kutokana na uamuzi huo Sophia atalazimika kupoteza ubunge. Ilielezwa kuwa amefukuzwa baada ya kupatikana na makosa ya maadili kinyume na Katiba na kanuni za chama hicho.
By: Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents