Habari

Madereva 18 kutoka Tanzania watekwa nchini Congo

Waasi wanaodaiwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamewateka madereva 21 wa Malori, wakiwemo Watanzania 18 wanaofanya kazi kwenye kampuni ya malori ya mizigo ya Alistair ya nchini Tanzania.

Tokeo la picha la Congo watekwa

Akithibitisha taarifa hizo Meneja usimamizi wa kampuni ya Alistair, Anna Joyce Mbise amesema madereva hao walitekwa asubuhi ya Juni 29, baada ya mapambano kati ya askari wa Serikali ya Congo na Waasi hao.

“Kwa mujibu wa maelezo ya madereva hao ni kwamba askari wa Serikali waliokuwa wanawasindikiza kabla ya msafara kuvamiwa, walizidiwa kwenye mashambulizi hayo ndipo wakatekwa,” amesema Mbise huku akiendelea kufafanua

“Wametueleza kuwa hakuna aliyejeruhiwa katika tukio hilo, waasi wamekuwa wakizungumza nao vyema, lakini gari zetu tatu zimeharibika kwa risasi kutokana na mashambulizi hayo,” amesema Mbise.

Hata hivyo tayari kampuni hiyo imewasiliana na viongozi husika wa Serikali kwa kuandika barua Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ili wawasaidie madereva hao kuachiwa huru wakiwa salama.

Tumejaza na hofu kuhusu usalama wao, kwani tunaamini kwamba askari wa jeshi la Serikali lazima wanajipanga kurejea kupambana ili kulikomboa eneo hilo, hapo tuna wasiwasi na usalama wa madereva hao ,” amesema Mbise kwenye mahojiano yake na Gazeti la Mwananchi.

Kwa upande mwingine Mratibu wa Shirikisho la Wasafirishaji Afrika Mashariki (FEARTA), Emmanuel Kakuyu amekubali kuwa taarifa hizo ni za kweli na wamezipata na kusema madereva hao walikumbwa na mkasa huo katika kijiji cha Lulimba kilichopo kati ya Ziwa Tanganyika na Kindu Manyema.

Kakuyu amesema waasi hao hawajawadhuru madereva, lakini alifafanua kuwa madereva watatu kati ya 21 wanatoka Uganda.

Watekaji wamekuwa wakizungumza nao vizuri ikiwamo kuwahakikishia usalama wao wakidai kwamba hawana ugomvi nao, bali wana ugomvi na Serikali ya Congo,” amesema Kakuyu.

Kaimu Mkurugenzi wa dawati la Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Suleiman Saleh alijibu kwa kifupi kwamba wamepokea taarifa za utekaji huo na tayari wameanza kushughulikia.

By Godfrey Mgallah

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents