Burudani

Mahakama kuisikiliza Tigo kuhusu fidia ya bilioni 2.1 za AY na Mwana FA

Mahakama ya Wilaya ya Ilala imekubali kusikiliza maombi ya kampuni ya Tigo, kuhusu fidia ya Sh2.1 bilioni ilizoamriwa kuwalipa wasanii maarufu wa muziki wa kizazi kipya, Hamisi Mwinyijuma na Ambwene Yesaya.

Mwana FA na AY

Mahakama imekubali kusikiliza maombi ya kampuni hiyo baada ya kutupilia mbali pingamizi la awali lililowekwa na wasanii hao, Mwinyijuma maarufu MwanaFA na Yesaya maarufu AY.

Mahakama hiyo Aprili 11, 2016 iliiamuru Tigo kuwalipa fidia ya kiasi hicho cha fedha wasanii hao kwa kosa la kukiuka Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, kwa kutumia kazi zao (nyimbo) kama miito ya simu bila ridhaa wala makubaliano nao.

Nyimbo hizo ni Usije mjini wa MwanaFA na Dakika moja wa AY. Kutokana na hukumu hiyo, wasanii hao walifungua maombi ya utekelezaji.

Hata hivyo, Tigo ilifungua maombi mahakamani hapo ikiiomba Mahakama iamuru kampuni ya Cellulant Tanzania Limited, ijumuishwe kwenye hukumu kama mmoja wa wadaiwa kwa kuwa wanataka nayo ijibu hoja za wadai.

Wakili Rosan Mbwambo anayeiwakilisha Tigo, amesema mteja wake aliingia makubaliano na Cellulant iwapelekee nyimbo na hakujua kama kampuni hiyo haikuwa na makubaliano na wahusika.

Ingawa katika kesi ya msingi kampuni hiyo ilikuwa mmoja wa wadaiwa, lakini hukumu haikuwataja jambo ambalo Tigo katika maombi yake inadai iliachwa kwa bahati mbaya.

Wasanii hao kupitia wakili Albert Msando waliweka pingamizi kuhusu maombi ya Tigo, wakiiomba Mahakama iyatupilie mbali.

Walidai kifungu cha 96 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai, kilichotumika kufungua maombi hakiiwezeshi Mahakama kutekeleza maombi hayo kwa sababu kosa la kutokuihusisha kampuni hiyo si la kiuandishi wala kihesabu.

Pia, walidai kama Tigo ilitaka kampuni hiyo iongezwe, ilipaswa kufungua maombi ya marejeo au kukata rufaa.

Akitoa uamuzi leo Jumatatu , Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ritha Tarimo amesema hoja hizo hazipaswi kuwasilishwa kama pingamizi. Amesema zitasikilizwa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo kama kampuni hiyo iliachwa kwa bahati mbaya au la.

Hakimu Tarimo amepanga kusikiliza maombi hayo Jumatano Oktoba 18.

Awali, Tigo ilifungua maombi Mahakama Kuu ikiomba kusimamisha utekelezaji wa hukumu.

Wasanii hao waliweka pingamizi na kushinda, ndipo walipofungua maombi ya utekelezaji wa hukumu hiyo.

Source: Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents