Habari

Mahimbali awapa siku 100 menejimenti ya GST kufanya mabadiliko

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali ameipa Siku 100 Menejimenti ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) zitakazomwezesha kuzifanyia kazi changamoto zilizoibuliwa na watumishi ikiwemo kufanya mageuzi ya kiutendaji ili hatimaye kuifanya kuwa taasisi shindani duniani.

Mahimbali aliyasema hayo Juni 25, 2024 wakati akizungumza na watumishi wa GST kwa niaba ya Waziri wa Madini katika kikao kilicholenga kusikiliza kero, changamoto wanazokabiliana nazo pamoja na kutoa mrejesho wa kikao cha awali kilichofanyika mwezi Aprili, 2024.

Mahimbali aliongeza kwamba, Wizara haina budi kuangalia kwa jicho la pekee taasisi ya GST ili iweze kuleta mabadiliko kutokana umuhimu wake katika Sekta ya Madini kwa kuwa ni taasisi inayotazamwa sana duniani kwa maendeleo ya Sekta.

Aidha, kikao hicho kilitoka na mapendekezo ya kukutana kila baada ya miezi mitatu ili kujadiliana masuala mbalimbali yanayoihusu taasisi hiyo, yote yakilenga kuhakikisha kwamba inaendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa majukumu yake ambayo kwa kiasi kikubwa yanagusa masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya Sekta ya Madini zikiwemo tafiti.

Kupitia Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri GST inatarajiwa kubeba maono hayo kwa nafasi kubwa katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa.

Aidha, katika Mwaka wa Fedha 2024/25 Wizara kupitia GST imepanga kununua helcopta kwa ajili ya kuongeza wigo wa shughuli za utafiti wa kina wa madini nchini.

Tanzania inajiandaa vilivyo kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 sehemu kubwa ya nchi iwe imefanyiwa utafiti wa kina kwa njia ya High Resolution Airborne Geophysical Survey kwa angalau asilimia 50 kutoka 16 iliyopo sasa huku GST ikitazamiwa kubeba jukumu hilo kwa asilimia 100.

Kupitia utafiti huo, Sekta ya Madini inatarajiwa kuzinufaisha sekta nyingine kiuchumi ikiwemo kilimo, nishati na maji kutokana na tafiti za kina zitakazofanyika huku madini muhimu na mkakati yakipewa nafasi kubwa ya kuwezesha mageuzi hayo kutokana na mahitaji yake kwa sasa duniani.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents