Habari

Makonda akanusha kuagiza msako nyumba za wageni mchana kweupe ‘serikali haiendeshwi na umbea’

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekanusha tetesi kuwa ametoa agizo la watu wanaolala kwenye nyumba za wageni wakamatwe nyakati za mchana na kudai kuwa serikali haiendeshwi kwa umbea.

makonda

Amekanusha uvumi huo uliosambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao mbalimbali ya kijamii na kuviasa vyombo vya habari kutoa habari zenye uhakika.

“Hili suala mimi nimelisikia katika namna ambayo hata mimi mwenyewe nimebaki nashangaa,” alisema Makonda. “Moja aliyetoa maelezo anasema nina umbea maana yake kwanza ni mmbea,kwasababu mbea lazima awe mbea. Lakini serikali haijawahi kufanya kazi kwa namna hii, serikali haiwezi kuendeshwa kwa njia ya umbea. Haiwezekani mtu anakaa kwenye gari yake anaanza kurekodi anatuma anaanza kuhangaisha vichwa vya watu wazima. Kwahiyo hata baadhi ya vyombo vilivyokwisha kuandika na baadhi ya watu kujadili ni kwamba wanajadili umbea ule ule tu. Ni namna pekee nzuri ya kupata wambea kwasababu ukiwa mbea utahangaika usiku na mchana kutafuta umbea, lakini serikali haifanyi kazi kwa umbea,” alisisitiza Makonda.

“Lakini la pili kufahamu ambalo ni jambo jema ni kwamba kabla ya kufanya maamuzi ya kuandika habari au kutangaza habari ni vema pia ukaonana na mamlaka husika, anasema polisi maana yake lazima kamanda Siro aulizwe na atoe taarifa, Je ni kweli kuna maagizo kama hayo? Lakini jambo jingine kama ni wakuu wa wilaya je kweli wakuu wa wilaya wamepokea maagizo kama hayo? Na hata kama ni mkuu wa mkoa je kuna maagizo kama hayo? Ukweli ni kwamba hakuna maagizo ya namna hiyo uamuzi wa mtu kupumzika ama kulala ni muda wowote ule. Wako watu wanafanya kazi ya ulinzi, wapo watu wanafanya kazi viwandani, wako watu wanasifiri na kuingia Dar usiku wa manane, kila mtu ana haki ya kupumzika na kila mtu ana haki ya kuwa na faragha yake, na ndiyo maana kukawepo na nyumba za kulala wageni.”

Aidha Makonda alitoa ufafanuzi wa suala la ukaguzi, “Sasa suala la ukaguzi au kama kuna maeneo wameonekana polisi wakifanya ukaguzi ni jambo jepesi tu. Nenda kwenye kituo husika utapewa maaelezo, na inawezekana labda wametilia shaka lakini ikumbukwe hivi karibuni askari watano wamepoteza maisha yao, sambamba na hilo juzi tumekamata silaha za kutosha na nyie mnafahamu, bastola zaidi ya 15,SMG zaidi ya nne na risasi nyingi sana na zimekamtwa kwenye majumba ya watu, inawezekana kuna baadhi ya maeneo wameyashtukia wakaona kuna haja ya kufanya upekuzi. Lakini si maelekezo zaidi ya usalama wa raia wote wanaoishi mkoa wa Dar es Salaam, hasa ikumbukwe kipindi cha nyuma nilisema wenyeviti wa mitaa wahafahamu wananchi wanaoishi nao, watu walilibadilisha jambo jingine,” alifafanua.

Pia amewataka wakazi wa Dar es Salaam watambue jambo hili, “mimi niwaombe wananchi wanaoishi mkoa wa Dar mamlaka zipo, viongozi wapo, hakuna mtu aneweza kubugudhiwa, cha msingi kila mtu aishi kwa utaratibu, sheria na kanuni, hatuwezi kuishi kwa maelekezo ya kila siku, tunaishi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni, taarifa zipuuzeni, na kwa bahati nzuri mmepata mkuu wa mkoa ambaye akiwa na jambo lake atalisema hadharani, hana sababu ya kumungu’nya maneno.”

“Wanaofanya kazi ya umbea waendelee, na tunaofanya kazi ya kujenga mkoa wetu tuendelee kujenga mkoa wetu kwa amani, upendo na mshikamano,na wanaofanya majungu na siasa waendelee, tunaofanya kazi za maendeleo tuendelee na mwisho wa siku Oktoba tarehe moja ni siku ya kupanda miti.”

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents