Habari

Mambo 16 yaliyotolewa na serikali kwa wabunge leo

Ijumaa hii Mei 25, 2018, Katika kipindi cha maswali na majibu bungeni Jijini Dodoma,wabunge mbalimbali wameuliza maswali na kujibiwa na serikali.

Kila wizara imejibu akiwemo Naibu Waziri wa Ardhi,Angeline Mabula, kwa Niaba ya Waziri wa Elimu,Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Mary Mwanjelwa,Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso na wengineo :Tazama mambo muhimu kwa ufupi yaliyotolewa na serikali:

Naibu Waziri wa Kilimo,Mary Mwanjelwa
# Katika mwaka wa fedha wa 2014/15 Serikali ilitoa ruzuku ya pembejeo kupitia vikundi vya wakulima na benki jamii badala ya utaratibu wa vocha za pembejeo uliokuwa unatumika awali.

# Wizara ya Kilimo ilipokea na kupitia nyaraka mbalimbali za makampuni na mawakala wa pembejeo 23 zenye madai ya jumla ya shilingi 7, 180, 914, 669.00, waliofanya kazi ya kusambaza pembejeo zenye ruzuku msimu wa kilimo mwaka 2014/15. Uhakiki wa awali umefanyika kwenye Mikoa 10.

# Kwa pembejeo zilizogawiwa kwa msimu wa mwaka 2016/17 ambapo Kampuni ya mbolea Tanzania ilipewa jukumu la kusambaza mbegu bora, uhakiki pamoja na ukaguzi wa mahesabu unaendelea.

# Serikali iliweka marufuku ya kilimo cha pamba katika baadhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Katavi ili kuzuia kuenea kwa mdudu anayeitwa funza mwekundu, zuio hilo ni mojawapo ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya kuzuia kuenea kwa wadudu hao.

# Taarifa ya wataalamu imebainisha kuwa funza mwekundu hayupo katika Mkoa wa Katavi.

# Serikali imetoa kibali cha kuruhusu zao la Pamba lizalishwe katika Wilaya ya Tanganyika na Mpanda Mkoani Katavi, na katika msimu wa 2017/18 uzalishaji umeanza katika wilaya hizo.

# Soko la korosho ghafi katika msimu wa 2017/2018 lilikuwa zuri hususani kutokana na kupanda kwa bei ya korosho na kuuzwa kuanzia shilingi 3500 hadi 4000 kwa kilo.

# Bei ya Korosho ilipanda kutokana na Serikali kuimarisha minada ya korosho na kuwahamasisha wanunuzi kutoka nchini Vietnam kuja kununua korosho moja kwa moja Tanzania badala ya kupata korosho hizo kupitia India.

# Hatua zilizochukuliwa na Serikali kutokana na kubainika kwa makontena 2 ya korosho ghafi zilizochanganywa na kokoto huko Vietnam, ni pamoja na kufanya uchunguzi wa kina na taarifa yake imewasilishwa katika vyombo husika kwa hatua za kisheria.

# Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu na kuhakikisha kuwa korosho zinazosafirishwa nje ya nchi zinakuwa na ubora unaostahili na kuwekewa nembo ya utambulisho .

# Uchunguzi unaofanywa sasa na vyombo vya dola umepelekea watuhumiwa kadhaa kukamatwa na kwa manufaa ya uchunguzi huo Serikali itatoa kauli mara itakapokuwa tayari kufanya hivyo.

Naibu Waziri wa Ardhi, Angeline Mabula, kwa Niaba ya Waziri wa Elimu

# Mtaala hutolewa kwa lengo la kuweka mwongozo mpana wa viwango vya utoaji elimu kwa kuzingatia idadi ya masomo yatakayofundishwa, umahiri utakaojengwa, njia za ufundishaji na ujifunzaji, vifaa vya ufundishaji, upimaji, ufuatiliaji na tathmini ya mtaala husika.

# Mtaala unaotumika katika shule za Serikali na shule binafsi ni mmoja na wanafunzi wote wanaosoma shule hizo hupata umahiri unaofanana. Aidha mitaala ambayo ni tofauti ni ile tu inayotumika katika shule chache za kimataifa zilizopo nchini, mitaala hii ya kimataifa imeruhusiwa ili kukidhi mahitaji ya raia wa kigeni wanaoishi hapa nchini.

Naibu Waziri wa Maji,Jumaa Aweso

# Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeziagiza Halmashauri zote nchini kuainisha maeneo yanayoweza kujengwa mabwawa na kutenga fedha kwenye bajeti zao kwa ajili ya kujenga angalau bwawa moja kwa mwaka.

# Utafiti wa maji hufanyika linapofanyika zoezi la kuyatambua maeneo yanayofaa kujengwa mabwawa ili kujua kiasi cha maji kinachoweza kuhifadhiwa katika mabwawa hayo ikilinganishwa na mahitaji.

#Hivyo, kazi hii ya utafiti wa maji yanayopotea kipindi cha mvua inaweza kufanyika sambamba na zoezi la kuainisha maeneo yanayofaa kujenga mabwawa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents