Picha/Video: Femina yazindua kipindi kipya cha Fema TV show
Wakati tukielekea kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2015, shirika la Femina Hip leo limetangaza kuanza kwa msimu mpya wa kipindi cha Fema TV.
Mtangazaji wa Fema TV Show, Rebeca Gyumi
Msimu huo umebeba jina la ‘Nguvu ya Binti’ ambao ni sehemu ya ajenda pana zaidi inayokwenda pia kwenye jarida la Fema ili kuhamasisha zaidi wasichana kujihusisha katika masuala ya uchaguzi.
Limmy Omary wa Fema TV Show (kulia) akizungumza kufafanua jambo mbele ya waandishi wa habari
Akizungumza na waandishi wa habari, mtangazaji wa kipindi hicho, Rebeca Gyumi alisema kipindi hicho kilicholenga kuelimisha wasichana kimeandaliwa kutoka kwenye mikoa mbalimbali ya Tanzania.
“Vipindi vitabeba ujumbe kwaajili ya wasichana wenyewe kuwahamasisha kushiriki michakato ya uchaguzi, kama haki na wajibu wao na kwamba wafanye hivyo kwa amani. Na uzalishaji wa kipindi umefanyika katika mikoa mbalimbali ya Tanzania ikiwemo Lindi, Njombe, Dodoma, Kigoma, Arusha na Dar es salaam,” alisema Rebeca.
Rebeca alisema kipindi hicho kitarushwa kwenye vituo vya runinga vya EATV na Star TV kila Jumapili na Jumatatu. Kipindi cha kwanza kitarushwa Jumapili hii, saa tatu kamili usiku kupitia EATV na Jumatatu, July 13 saa tatu na nusu usiku kupitia Star TV.
Alisema kama kawaida ya Fema Hip, burudani na elimu vitaenda sambamba na kwamba mfumo wa uwasilishaji wa kipindi umebadilika ili kuruhusu wadau zaidi kushiriki. Pia kwakuwa ni msimu mpya unaohusu nguvu ya binti, watangazaji ni mabinti wenye nguvu watakaokuwa zaidi ya watangazaji. Kutakuwepo na zawadi na vituko vya Bwana Ishi.
Team Nguvu ya binti wakiwa katika ubora wao
Waandishi wa habari wakichukua matukio