Habari

RC Makonda awaongezea muda wauza magari kuhamia Kigamboni

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda amesema mpaka kufikia mwezi Oktoba mwaka huu hataki kuona magari yakiuzwa sehemu nyingine katika jiji la Dar es salaam isipokuwa Kigamboni ambako wafanyabiashara wa magari walitakiwa kuhamia mwezi huu.

RC Makonda (kushoto) akinena jambo na moja ya wafanyabiashara ya magari.

Akiongea na Wafanyabiashara wa magari ofisini kwake leo Jumatano Januari 24, RC Makonda amesema ameongeza muda kutokana na maombi ya wafanyabiashara hao kudai kuwa waongezewe muda hadi Septemba ili wajipange zaidi kuhamia Kigamboni katika eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya biashara ya magari.

Najua Septemba ni mbali sana lakini siyo mbali. Siku zote muda huwa hautoshi hata ukiongezwa hautumiki vizuri. Sasa ikifika Oktoba 1, sitaki kuona ‘showroom’ yoyote huko mitaani,”amesema RC Makonda.

Akifafanua juu ya eneo hilo lililotengwa kwa ajili ya biashara ya magari, RC Makonda amesema wafanyabiashara watakaonunua maeneo katika eneo hilo watapata punguzo la bei la asilimia 25 na watatakiwa kulipa malipo hayo ndani ya miaka sita.

Kuhusu suala la miundombinu RC Makonda amesema “tutahakikisha kwamba miundombinu muhimu na mazingira wezeshi vinapatikana. Hii ni pamoja na maji, umeme, barabara, usalama na uwepo wa taasisi zinazohusika na biashara kama vile TRA,”.

Hatua hiyo ya kuhamia Kigamboni imeungwa mkono na wafanyabiashara wengi wakidai kuwa italeta faida na wateja wao watapata bidhaa za uhakika.

“Wafanyabiashara tutakuwa na mazingira mazuri ya biashara, kama ulikuwa unaagiza magari 80 kwa mwezi, unaagiza 200. Biashara itakuwa na ushindani mkubwa,”amesema Mkurugenzi wa Kampuni ya Chicago General Traders, Salim Chicago ambaye pia muakilishi wa wafanyabiashara wa magari.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents